SIKU 90 ZA DG TANTRADE: ATOA MWELEKEO WA TAASISI KWA MIAKA MITANO IJAYO
- November 6, 2026
06 Novemba 2026, Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Ephraim Balozi Mafuru, ameeleza mwelekeo wa taasisi kwa miaka mitano ijayo katika kikao chake cha kwanza na watumishi wote baada ya kutimiza siku 90 tangu kuanza kuiongoza Mamlaka hiyo. Kikao hicho kimefanyika leo Makao Makuu ya TanTrade, ambapo amesisitiza kuimarisha huduma kwa wafanyabiashara na kufanya maonesho kuwa nyenzo yenye matokeo katika kufungua masoko ya bidhaa na huduma za Tanzania.
Akizungumza katika kikao hicho, Mafuru amesema TanTrade itaboresha na kufanya kuwa ya kisasa mifumo ya kuratibu na kuendesha maonesho ya biashara ndani na nje ya nchi, ili kuongeza ufanisi na kuimarisha uhusiano kati ya wazalishaji na wanunuzi. Ameeleza kuwa taasisi itajikita katika kuwajengea uwezo wafanyabiashara kuongeza thamani ya bidhaa na huduma zao, kujenga chapa imara na kuuza bidhaa zenye ubora unaokidhi mahitaji ya masoko ya ndani na kimataifa.
Aidha, amewataka watumishi kuelewa vipaumbele vya taasisi na nafasi ya kila mmoja katika kuvitekeleza, huku wakizingatia uwajibikaji, nidhamu na weledi. Amesisitiza kuwa kila mtumishi anapaswa kujipima kwa matokeo ya kazi yake na kutumia ujuzi alionao kukuza biashara, akibainisha kuwa mafanikio ya TanTrade yanategemea ushirikiano na mchango wa kila mmoja katika kuwezesha biashara na kupanua fursa za masoko.
Katika kikao hicho, watumishi walipata fursa ya kuuliza maswali, kutoa maoni na kufanya majadiliano na Mkurugenzi Mkuu kuhusu mwelekeo wa taasisi. Kupitia majadiliano hayo, Mafuru amefafanua namna vipaumbele vya TanTrade vinavyotafsiri Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku, hususan kuwezesha uongezaji thamani, kuimarisha ushindani wa bidhaa na huduma za Tanzania na kuongeza ushiriki wa wafanyabiashara katika masoko ya kimataifa.
Kikao hicho kimewashirikisha watumishi wa Makao Makuu pamoja na wale wa Ofisi ya Zanzibar na Ofisi za Kanda za Mwanza, Arusha, Dodoma na Kigoma walioshiriki kwa njia ya mtandao. Mafuru amewashukuru watumishi kwa mapokezi mazuri na utayari wa kushirikiana, huku akiwahimiza kuwa na uelewa na dhamira ya pamoja katika kutekeleza mwelekeo huo wa miaka mitano kwa manufaa ya wafanyabiashara na uchumi wa Taifa.