NAIBU WAZIRI WA MADINI AHIMIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA NA UONGEZAJI THAMANI GEITA
- September 27, 2026
27 Septemba, 2026 - Geita
Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kisurwa, amewataka wadau wa sekta ya madini kutumia Maonesho ya 9 ya Teknolojia ya Madini Geita kujenga mahusiano ya kibiashara, kukuza matumizi ya teknolojia na kuongeza thamani ya madini kwa manufaa ya Taifa.
Akifungua maonesho hayo katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Dkt. Kisurwa amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali, wachimbaji, wafanyabiashara, wawekezaji na watoa huduma ni muhimu katika kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye uchumi. “Madini ni utajiri, tuwajibike kwa pamoja kufikia Dira ya Taifa 2050,” amesema.
Ufunguzi huo umehudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Alexander Mnyeti; Katibu Tawala wa Mkoa, Mohamed Gombati; Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Latifa M. Khamis; na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Fredy Liundi, pamoja na wadau wengine wa sekta ya madini.
Maonesho hayo yenye kaulimbiu “Madini ni Utajiri, Tuwajibike kwa Pamoja Kufikia Dira ya Taifa 2050” yanaendelea hadi tarehe 3 Oktoba 2026.