MKUTANO WA 153 IPU KUIMARISHA UHUSIANO WA TANTRADE NA WADAU WA BIASHARA KUTOKA MATAIFA YA NJE
- October 11, 2026
05 Oktoba, 2026 - Arusha
Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) umekuwa fursa muhimu kwa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kuimarisha uhusiano na kushirikiana na wadau mbalimbali wa biashara kutoka mataifa ya nje, kwa lengo la kutangaza fursa za biashara na uwekezaji zilizopo nchini Tanzania.
Mkutano huo unafanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC), jijini Arusha, kuanzia leo tarehe 5 hadi 9 Oktoba 2026, ukiwakutanisha wawakilishi wa mabunge kutoka mataifa mbalimbali duniani pamoja na wadau wanaoshiriki katika shughuli za maendeleo na ushirikiano wa kimataifa.
Katika Mkutano huo, TanTrade inashiriki katika Maonesho madogo yanayoenda sambamba na jukwaa hilo, ambapo kupitia banda lake imepata fursa ya kuwasiliana na wabunge, wawakilishi wa mabunge, wafanyabiashara na wadau wengine kutoka mataifa shiriki, huku ikitoa taarifa kuhusu bidhaa zinazozalishwa nchini, fursa za masoko, uwepo na matumizi ya nembo ya Made in Tanzania inayotambulisha ubora wa bidhaa zinazozalishwa Tanzania, pamoja na huduma zinazotolewa na Mamlaka katika kuwawezesha wafanyabiashara na wajasiriamali wa Tanzania kufikia masoko ya ndani na nje ya nchi.
Aidha, ushiriki wa TanTrade katika mkutano huo unatoa nafasi ya kujenga na kuimarisha mitandao ya kibiashara kati ya Tanzania na mataifa mbalimbali, pamoja na kufungua milango ya fursa mpya za biashara kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wa Tanzania kupitia mahusiano na mitandao ya kimataifa.