Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeipongeza Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania TanTrade

  • August 16, 2023

KAMATI YAIPONGEZA TANTRADE KWA KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA 

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeipongeza  Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania TanTrade kwa kuboresha mazingira ya biashara hususani Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) 2023.

Vilevile Kamati hiyo imeiagiza TanTrade kupitia Sheria na kuwa na mikakati mahususi  ikiwemo ya uboreshaji wa miundombinu  katika maonesho ya sabasaba na utafutaji wa masoko kwa bidhaa za Tanzania inayoendana na wakati na mabadiliko ya Teknolojia

Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti  wa Kamati hiyo Mhe. Mariam Ditopile (Mb.) Agosti 15, 2023 wakati ikipokea Taarifa ya Hali Halisi ya Utendaji wa Majukumu ya TanTrade katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.

Aidha, wajumbe hao walipata fursa ya kutoa  maoni mbalimbali kuhusu uendelezaji wa biashara hususan mauzo ya nje, utafutaji wa masoko, biashara mtandao na mapendekezo ya kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika ukuzaji wa  biashara  

Naye Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe(Mb.) akijumuisha maoni na mapendekezo hayo ameihakikishia Kamati hiyo kuwa maelekezo na mapendekezo yote yaliyotolewa na Kamati hiyo yatatekelezwa  ili kuendelea kuweka mazingira mazuri ya biashara, kukuza biashara na mauzo ya ndani na nje   na hatimaye kukuza uchumi wa nchi.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara aliieleza Kamati hiyo kuwa Wizara imeanza kupitia na kurekebisha Sera na Sheria mbalimbali ikiwemo Sheria inayosimamia TanTrade ili ziendane na wakati na mabadiliko ya teknolojia

Awali Mkurugenzi  Mkuu wa TanTrade Bi Latifa Mohamed  akiwasilisha taarifa ya Taasisi yake kwa Kamati hiyo, amesema jukumu kuu la TanTrade ni kukuza na  kuendeleza biashara ya ndani na nje ya nchi ili kuimarisha biashara yenye tija katika maendeleo ya kiuchumi nchini.