Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

TanTrade Yajipanga Kusaka Masoko ya Bidhaa za Tanzania Kimataifa

  • September 5, 2023

Na Beatrice Sanga - MAELEZO
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imesema itaendelea kusimamia sera na miongozo mbalimbali ya kimaendeleo ili kuleta tija nchini kupitia shughuli mbalimbali ikiwemo kuratibu maonesho ya biashara, misafara na mikutano ya wafanyabiashara, nakutafiti masoko mbalimbali kwaajili ya kukuza thamani ya bidhaa za ndani na kuongeza ushindani na bidhaa zinazozalishwa nje ya nchi.
 
Hayo yamebainishwa leo Septemba 4, 2023 na Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Latifa Khamis wakati wa Mkutano wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mamlaka hiyo na wahariri wa Vyombo vya habari Jijini Dar es Salaam huku akieleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023, TanTrade imefanikiwa kuratibu matukio mbalimbali ikiwemo programu za utafiti, makongamano na misafara ya kibiashara, maonesho na mikutano ya kuunganisha wazalishaji na wanunuzi ambayo yameongeza makusanyo katika mfuko wa Hazina kwa asilimia 20.15 kwa kipindi cha miaka mitano.
 
Mkurugenzi huyo amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano, Tantrade ilifanikisha kusainiwa kwa jumla ya mikataba 46 yenye thamani ya shilingi trilioni 17.53.
 
“Katika Kipindi cha miaka mitano (5) TanTrade ilipanga kukusanya jumla ya shilingi 52,562,298,340 na imefanikiwa kukusanya shilingi 40,004,650,548 sawa na asilimia 76, kutoka vyanzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ruzuku kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya mishahara na miradi ya maendeleo na vyanzo vya mapato ya ndani ikiwemo ada inayotozwa kwenye uratibu na usimamizi wa maonesho, upangaji wakati usio wa maonesho pamoja na ushiriki na viingilio vya maonesho ya DITF,” amesema Bi. Latifa
 
Aidha Latifa amesema kuwa maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba ambayo yamekuwa yakifanyika kila mwaka yamezidi kuongeza thamani yake kwa kipindi cha miaka mitano, ambapo kampuni za ndani na nje, washiriki, idadi ya nchi zilizoshiriki maonesho hayo, watembelea maonesho pamoja na ajira zilizozalishwa vimeongezeka na hivyo yamezidi kuongeza wigo wa biashara za ndani na nje ya nchi.
 
Mkurugenzi huyo amesema kutokana na mafanikio hayo, “TanTrade imekamilisha maombi ya ufadhili ya kuendeleza rajamu (Branding) ya Taifa ya Viungo (Tanzania Spice Label) kwa kushirikiana na Kituo cha Biashara cha Kimataifa (ITC) pamoja na wadau wa sekta ya viungo, ambapo hadi Agosti, 2023 TanTrade imekamilisha rajamu ya iliki, tangawizi, mdalasini, pilipili manga na karafuu. vilevile, mamlaka inaendelea na taratibu za kukamilisha rajamu za bidhaa nyingine ikiwemo asali, korosho, kahawa na chai pamoja na mafunzo kwa wafanyabiashara 6,979 kupitia programu 26 ili kuimarisha uwezo wa kujiendesha kiushindani.”
 
Aidha Tantrade imeendelea kusaka masoko nje ya nchi ya bidhaa mbalimbali zinazolishwa nchini ikiwemo mazao ya biashara na madini ili ziendelee kuongeza wigo wa uzalishwaji na kuongeza thamani ya mnyororo kwa wazalishaji lakini pia kuongeza fedha za kigeni ambapo mazao na madini hayo ni pamoja na Dhahabu, Korosho, Ufuta, Mbaazi, Kahawa, Dengu, Almasi, vifungashio vya mifuko, Pamba, mazao mengine ni Karafuu, Mchele, Soya, Karanga, Parachichi, Pilipili Muhogo, Mahindi, Karafuu,
Asali, Mbegu Za Maboga, Korosho, Zabibu, Nyama.