SERIKALI YAENDELEA KUBORESHA HUDUMA ZA TEHAMA NCHINI.
- July 25, 2023

………………….
Na. Norah Thomas-TanTrade Dar es salaam.
Dar es salaam
8 Julai, 2023.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye tarehe 8 Julai, 2023 ameyasema hayo, wakati akifungua rasmi siku maalum ya TEHAMA iliyofanyika katika Uwanja wa Maonesho wa Mwl. JK Nyerere barabara ya Kilwa Dar es salaam. Mhe. Nape, amewataka Wananchi kuendelea kutumia kila fursa ya TEHAMA sambamba na kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kuboresha huduma za TEHAMA, lengo hasa ikiwa ni kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa Kidijitali.
Aidha Mhe. Nape akiwa ameambatana na Naibu waziri Wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Methew (Mb), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Selestine Gervas Kakele pamoja na Mkurugenzi wa Utawala na Usimazi wa Rasilimaliwatu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bi. Salome Kessy ameeleza mikakati mbalimbali inayoendelea kufanywa na Serikali ya Tanzania katika kufanikisha Tanzania kuwa na Uchumi wa kidijitali.
Pia ameipongeza TanTrade kwa kuonyesha juhudi za kumsapoti Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hasan na kufanya mapinduzi ya kuboresha Maonesho na kuwafanya Wafanyabiashara pamoja na Watembeleaji kufurahia Maonesho haya ya 47, na kuhaidi Wizara yake itashirikiana na TanTrade katika kuboresha miundo mbinu ya TEHAMA kwa Maonesho yajayo.
‘’Baada ya Maonesho haya ya mwaka huu, Katibu Mkuu na Taasisi zetu za Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia tutakaa na TanTrade ili tufanye tathmini ya pamoja tuone yale maeneo ambayo tunaweza kuboresha miundo mbinu ya TEHAMA na kuyafanya maonesho yajayo yawe bora zaidi’’.Alisema.
Pamoja na maazimisho ya siku hiyo, Mhe. Nape amezindua huduma ya Intaneti ya Wazi (Free-Wifi) katika maeneo 17 ndani ya Uwanja wa Maonesho ya Sabasaba), Huduma hiyo ya wazi imewezeshwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa kushirikiana na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).
Vilevile, Mhe. Waziri Nape ametumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali ya awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa Wizara hii yenye lengo la kurahisisha huduma za TEHAMA nchini.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade Bi. Latifa M. Khamis ameishukuru Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia mtandao wa TTCL kwa kutoa huduma ya Intaneti ya wazi (Free wifi) katika Maonesho hayo kwani huduma hiyo imelenga kurahisisha Mawasiliano na kuboresha Maonesho yawe na mvuto zaidi na kuwasaidia Washiriki pamoja na Watembeleaji kuweza kupata Mawasiliano kwa njia rahisi na kwa haraka zaidi katika kipindi chote cha Maonesho, pia ameelezea namna ambavyo TanTrade inafanya kazi zake kulingana na mabadiliko ya Teknnolojia kwa kuzindua mifumo mipya mbalimbali ya kigitali ambayo imetumika katika Maonesho ya 47.
‘’ Teknolojia ni kipaumbele katika utendaji wetu wa kazi Hatupo nyuma katika Mabadiliko ya teknolojia ili kurahisisha shughuli za ufanyaji wa Biashara nchini tumetumia mifumo mipya mbali ambayo ni pamoja na mfumo wa kidigitali wa ugawaji wa nafasi za mabanda , mfumo wa kidigitali wa ugawaji wa vitambulisho pamoja na mfumo wa kugawa tiketi za kuingia katika Uwanja wa Maonesho.’’ Alisema.
Pia Bi. Latifa aliwapongeza Waandishi wa habari kwa kusapoti na kuyatangaza Maonesho ndani na nje ya nchi.