Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

HAFLA YA HITIMISHO LA SIKU 179 ZA KUPEPERUSHA BENDERA YA TANZANIA KWENYE MAONESHO YA EXPO2023 DOHA YAFANYIKA.

  • March 29, 2024

28 Machi, 2024
Doha, Qatar

Maonesho ya Kimataifa ya mbogamboga na matunda (Horticultural Expo) ambayo pia yanafahamika kama Expo2023 Doha yaliyoanza rasmi tarehe 2 Oktoba 2023 yamemalizika tarehe 28 Machi 2024 katika Mji wa Doha nchini Qatar ambazo ni jumla ya siku 179. Kwa upande wa Tanzania, hafla ya kufunga rasmi Maonesho haya ilihudhuriwa na Mhe. Habibu Awesi Mohamed, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Qatar na Bi. Latifa Mohamed Khamis, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade).

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara chini ya uratibu wa  Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar iliratibu ushiriki wa nchi kwenye maonesho haya ili kuweza kutumia vyema fursa mbalimbali za kilimo, biashara, utalii na uwekezaji zilizopo kwenye nchi zilizoshiriki kwenye Maonesho haya.

Katika maonesho haya, TanTrade imeratibu ushiriki wa Wizara, Taasisi, na wajasiriamali kutoka Tanzania pamoja na jumuiya ya watanzania waishio Qatar ambao walipata fursa ya kuonesha utajiri wa bidhaa mbalimbali zenye ubora kwa watembeleaji zaidi ya milioni 4 kutoka mataifa 77 yaliyoshiriki katika Maonesho haya. Bidhaa zilizooneshwa katika Maonesho haya ni kahawa, chai, korosho, viungo, matunda makavu, nafaka, bidhaa za mikono na nyingine nyingi.

Aidha, Maonesho haya yamekuwa fursa na kuleta mafanikio kwenye maeneo mbalimbali Tanzania hasa katika kuhakikisha bidhaa zetu zinapenya katika masoko ya nchi za ukanda wa ghuba (Gulf countries), wawekezaji kuonesha nia ya kuja nchini Tanzania kwa ajili ya kuona maeneo wanayoweza kuwekeza pamoja na wafanyabiashara walioonesha nia ya kununua bidhaa za Tanzania na kuuza katika nchi zao.

Mafanikio mengine yaliyopatikana ni watembeleaji wengi kuvutiwa na kufanya ziara za kitalii katika maeneo mbalimbali ya vivutio vya kitalii nchini vikiwepo Visiwa vya Zanzibar, Hifadhi za taifa za Serengeti, Ngorongoro na Manyara.

Baada ya kumalizika kwa Maonesho haya, TanTrade inaendelea kutafuta fursa nyingine za masoko ya bidhaa za wafanyabiashara wa Tanzania kupitia Maonesho makubwa ya Dunia ya Expo2025 Osaka yanayotarajiwa kufanyika kuanzia mwezi Aprili hadi Oktoba 2025. Endelea kutembelea kurasa zetu za mitandao ya kijamii ili kupata taarifa zaidi ya fursa hii na nyingine nyingi.