Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

TANTRADE, UBALOZI WA UINGEREZA WARATIBU MAONESHO YA SEKTA BINAFSI KWA MAKAMPUNI YA UINGEREZA .

  • July 21, 2023



Na. Norah Thomas-Dar es salaam.
10 Mei, 2023.

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Uingereza wameratibu maonesho kwa kampuni za sekta binafsi kutoka Uingereza yaliyoshirikisha zaidi ya washiriki 50 ambayo yanasimamiwa na British Business Group (BBG).

Maonesho hayo yamefanyika Mei 10, 2023 katika Hotel ya Coral Beach jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuonesha na kutangaza bidhaa zinazozalishwa na kampuni hizo zilizopo nchini Tanzania.

Akizungumza katika maonesho hayo Mjumbe wa Waziri Mkuu wa Uingereza katika Uwekezaji na Biashara nchini Tanzania, Lord John Walney ameishukuru Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara na TanTrade kwa kuendelea kuboresha sekta ya uwekezaji na kuvutia kampuni nyingi zaidi kutoka nchi mbalimbali duniani ikiwemo Uingereza kuja kuwekeza nchini Tanzania.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Ukuzaji Biashara kutoka TanTrade Bw. Fortunatus Mhambe  amefafanua kuwa British Business Group Tanzania, ni kundi la watu wanaofanya kazi pamoja na wadau wengine wa asasi za kiraia kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Hivyo amesema TanTrade imefika kwa ajili ya kuwaunga mkono kwani ni wadau muhimu ambao wanasaidia katika kuchochea maendeleo na kukuza biashara na uchumi wa Tanzania.

Pia aliwaalika Wafanyabiashara kushiriki katika Maonesho ya Biashara ya 47 ya Kimataifa Dar e s Salaam (DIFT) yatakayoanza kuanzia tarehe 28 Juni hadi 13 Julai , 2023 kwenye Uwanja wa Maonesho wa Mwl. J.K Nyerere SabaSaba.