Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

TANTRADE YAWAONYA WANAOFANYA MAONESHO NA MISAFARA YA BIASHARA BILA KIBALI

  • September 6, 2023

Tarehe 4 September, 2023
Dar es Salaam

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imezungumzia kuhusu uwepo wa Maonesho na Makongamano mengi ya Kibiashara ambayo hayajaidhinishwa na TanTrade yanafanyika nchini Tanzania.

Akizungumza katika Mkutano na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Bi. Latifa Khamis alisema kuwa TanTrade itachukua hatua kali kwa wanaoratibu Matukio ya Ukuzaji Biashara bila kuomba kibali ambapo imepelekea wengine kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kwa kutumia picha za watu mashuhuri nchini ikiwemo Mawaziri ili kuwavutia wahudhuriaji na kuvuta umati wa watu kushiriki matukio yao. Mkurugenzi huyo alisisitiza waaandaaji wote wa Maonesho au Makongamano kupata kibali kutoka TanTrade kama Taasisi ya Serikali yenye dhamana ya kusimamia tasnia ya maonesho na matukio yote ya kukuza biashara.

Pia alifichua uwepo wa waandaaji wa ziara za kibiashara nje ya nchi bila kibali na kupeleka wafanyabiashara kwa kisingizio cha kuwakilisha Tanzania. Ambapo hii ni kinyume na taratibu na wengine wamekuwa sio waaminifu. " Hii inahatarisha na kuchafua taswira ya nchi yetu na mazingira yake ya biashara kwa ujumla”- amesema Bi. Latifa Khamis.

TanTrade inawakaribisha waandaaji wote na wenye nia ya kuandaa matukio ya kukuza biashara katika Ofisi zake ili wapatiwe vibali pamoja na msaada wa namna bora ya kuandaa matukio hayo ili yalete tija kwa sekta ya biashara na kulinda taswira ya nchi na diplomasia ya kibiashara baina ya Tanzania na nchi nyingine.