Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

TANTRADE YATOA MAFUNZO KWA WAFANYABIASHARA WA MKOA RUVUMA KUHUSU FURSA ZILIZOPO KATIKA SOKO HURU LA AFRIKA

  • September 3, 2023

..........................
SONGEA-RUVUMA
30 AGOST, 2023.


WAFANYABIASHARA wa Mkoa wa Ruvuma wamejengewa ufahamu kuhusu fursa zilizopo katika Soko huru la Afrika (AfCFTA) ili kupata uelewa na kuhamasika kutumia  soko hilo na kuuza bidhaa kutokea Tanzania.

Mafunzo hayo yameratibiwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia  Taasisi ya TanTrade na kufanyika kwenye Ukumbi wa Manispaa ya Songea na  kufunguliwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Bw. Joel Mbewa.

Akizungumza kabla ya kufungua mafunzo hayo Katibu Tawala amelitaja lengo la mafunzo hayo kuwa ni mikakati ya kutumia fursa za kimasoko zilizopo katika eneo huru la biashara barani Afrika kwa bidhaa zinazozalishwa Nchini.

Amezitaja faida za mafunzo hayo kwa wafanyabiashara mkoani Ruvuma kuwa ni wafanya biashara kupata uelewa wa kutosha juu ya fursa  zinazopatikana katika sekta wanazofanyia kazi na kukua kwa idadi ya bidhaa zinazouzwa katika soko hilo kutokea Tanzania.

Faida nyingine za mafunzo hayo amezitaja kuwa ni kuboresha bidhaa zinazozalishwa ili kukabiliana na ushindani uliopo katika soko huru la Afrika,kuongezeka kwa bidhaa zinazozalishwa na kumiliki soko husika na kupata wanunuzi wa malighafi zilizopo mashambani kutokana na kuwepo kwa soko la kutosha.

“Ni Imani yangu mafunzo haya yatawajengea uelewa mkubwa katika kutumia fursa hizo ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla’’,alisisitiza.

Katika Mafunzo hayo TANTRADE imelitaja eneo la Biashara Huru la Bara la Afrika (AfCFTA) kuwa ndilo eneo kubwa zaidi la biashara huria duniani linaloleta Pamoja nchi 55 za Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya nane za kiuchumi za kikanda ili kuunda soko moja la bara la Afrika.

Imeelezwa kuwa Tanzania ni Mwanachama rasmi wa AfCFTA toka mwaka 2021 ikiungana na nchi nyingine  za Soko Huru la Afrika.

Zimetajwa  nchi hizo kuwa ni Ghana, Kenya, Rwanda, Chad,Swaziland,Guinea,Mali,Namibia,Afrika ya Kusini, Jibouti, Mauritania, Uganda, Senegal, Kongo DRC,Togo, Misri, Ethiopia, Gambia, Sieraleone, Zimbabwe, Burkinafaso, Garbon, Equatorial Guineana Sao Tome.

 TanTrade imetoa wito kwa wafanya biashara wa Mkoa wa Ruvuma kuhakikisha wanatangaza biashara zao kwenye maonesho ya kimataifa kama Sabasaba ili kujitangaza kimataifa.

Awali wafanyabiashara hao waliipongeza serikali kwa kuboresha miundombinu ya barabara,majini na angani katika Mkoa wa Ruvuma hali ambayo inarahisisha utendaji kazi katika biashara zao.

Hata hivyo walizitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili kuwa ni Pamoja na kuchelewa malipo ya bidhaa zao kama mazao,ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu biashara na changamoto ya leseni ya biashara.

Uongozi wa Mkoa wa Ruvuma na Taasisi ya TanTrade imeahidi kuzitafutia ufumbuzi changamoto za wafanyabiashara ili waweze kufanya biashara zao kwa ufanisi  na kulifikia soko huru la Afrika kama ilivyo kwa wafanyabiashara katika nchi nyingine.