Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

TANTRADE YAWASILISHA MAUDHUI YA MUONEKANO WA BANDA LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE MAONESHO MAKUBWA YA DUNIA YA OSAKA 2025 (EXPO2025 OSAKA)

  • October 13, 2023

LEO 13 OKTOBA 2023 OSAKA, JAPAN

Mamlaka ya Maendeleo na Biashara Tanzania (TanTrade) imeshiriki katika programu ya washiriki wa banda la pamoja kwenye Maonesho makubwa ya dunia ya Osaka 2025 (Expo2025 Osaka) yanayotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 13 Aprili hadi 13 Oktoba, 2025 katika Mji wa Osaka, Japan.

Programu hiyo inayofanyika kuanzia tarehe 11-18 Oktoba 2023 imeandaliwa na Shirika la Ushirikiano la Japan (JICA) imelenga kuzisaidia nchi zinazoendelea kujipanga vyema kwenye maandalizi ya ushiriki wao kwenye Maonesho haya ambayo yanatarajiwa kuhudhuriwa na zaidi ya nchi 150 duniani na watu zaidi ya Milioni thelathini wakikadiriwa kutembelea Maonesho hayo  kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Maonesho ya Expo2025 Osaka yana kaulimbiu inayosema “Designing future society for our lives” (Kutengeneza jamii ya baadae kwa maisha yetu) ikiwa na lengo la kufanya jamii ulimwenguni kote kufikiria namna bora inavyohitaji kuishi na namna itakavyotumia uwezo wake katika kuinua maisha yao. Kaulimbiu hii imeandaliwa mahususi baada ya wimbi la mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO-19 ambapo jamii nyingi zilipoteza umoja na ushirikiano na kushuka kwa maisha; hivyo maonesho haya yanalenga kuileta pamoja jamii baada ya janga la UVIKO-19. Kaulimbiu ndogo za Maonesho haya ni ‘‘Saving lives’’, (Kuokoa Maisha), ‘‘Empowering lives’’ (kuwezesha maisha) na ‘‘Connecting Lives’’ (Kuunganisha Maisha).

Tanzania itashiriki Maonesho haya chini ya Kaulimbiu ndogo ya “Kuunganisha Maisha” (Connecting Lives) ambayo inalenga kuionesha dunia namna ambavyo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo kwa kuishirikisha jamii yote kwa usawa na kwa maslahi mapana ya nchi. Katika kuitekeleza kaulimbiu ndogo hii, Tanzania imeandaa Kaulimbiu yake ndogo ambayo inasema “Better life Better tomorrow” ikiwa inalenga kuionesha dunia namna ambavyo serikali inafanya jitihada za kuboresha sekta za kijamii na kiuchumi kwa ajili ya maisha bora ya baadae kwa watanzania.

Pamoja na mambo mengine, TanTrade imewasilisha maudhui ya banda la Tanzania kwa kuonesha mambo yatakayooneshwa wakati wa siku zote 179 za Maonesho haya. Banda la Tanzania litaonesha namna Lugha ya Kiswahili inavyotumika kuwaunganisha na kuwaleta kwa pamoja zaidi ya watanzania milioni sitini wenye lugha zao za asili zaidi ya 126, Vivutio mbalimbali vya utalii kutoka Tanzania bara na Zanzibar, programu mbalimbali za vijana na wanawake, maboresho ya sekta ya afya na fursa mbalimbali za Biashara na uwekezaji.

Programu hii inatarajiwa kufungwa rasmi tarehe 18 Oktoba 2023.