Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

TANTRADE YASHIRIKI KONGAMANO LA BIASHARA NA UWEKEZAJI KATI YA CHINA NA TANZANIA

  • July 21, 2023

Na. Norah Thomas- TanTrade Dar es salaam.
25 April, 2023

Kaimu Mkurugenzi Ukuzaji Biashara wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) Bw. Fortunatus Mhambe aelezea fursa mbalimbali za Biashara nchini kwa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa China.

Bw. Mhambe aliyasema hayo tarehe 25 Aprili, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) katika Kongamano la Biashara kati ya China(Shenzhen Nanshan)-Tanzania (Dar-es-Salaam) kuhusu Uchumi na Biashara.

Bw. Mhambe alielezea kuhusu hali ya kibiashara baina ya nchi hizo mbili na umuhimu wa kuwa na Biashara linganifu ambapo kwa sasa Tanzania inaagiza kwa wingi bidhaa za viwandani na kuiuzia nchi hiyo bidhaa za Kilimo kwa kiasi kidogo tu ukilinganisha na fursa kubwa iliyopo ya kuuza bidhaa za kilimo katika nchi hiyo ambayo ni moja ya nchi zenye uchumi mkubwa duniani.

Kadhalika, Bw. Mhambe mwisho aliwakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka China kushiriki kwenye Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar Es Salaam alimaarufu Sabasaba yatakayofanyika kuanzia tarehe 28 Juni - 13 Julai, 2023 katika Uwanja wa Maonesho wa Mwl. J. K. Nyerere, Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam na kuwawezesha wafanyabiashara hao kutangaza bidhaa na teknolojia zinazozalishwa nchini humo pamoja na kuwawezesha Wawekezaji kutoka China kuweza kuzitambua fursa mbalimbali za Uwekezaji zinazopatikana nchini.

Kwa upande wake Mayor wa jiji la Nashan Bw. Huang Xiangyue aliipongeza TanTrade kwa kutoa fursa hiyo na kuahidi kushiriki Maonesho hayo kwa makampuni ya Teknolojia ya Huawei na Tekno kwenye Banda la TEHAMA.

Aidha, kwa upande wa Mkurugenzi wa Uwekezaji kutoka Ofisi ya Rais Bw. Aritides R. Mbwasi ambaye alikuwa anamwakilisha Katibu Mkuu Uwekezaji Dkt. Tausi Mbaga Kida alipongeza kazi kubwa inayofanywa na TANTRADE na TIC na kuwakaribisha wawekezaji hao kutumia taasisi hizo ili kuwawezesha kufikia malengo yao ya Biashara na Uwekezaji nchini.