TANTRADE YASHIRIKI UZINDUZI WA MRADI WA VIATU VYA SHULE
- September 4, 2025

Dar es Salaam,
2 Septemba, 2025.
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeshiriki Uzinduzi wa Mradi wa viatu vya ngozi vya shule, unaosimamiwa na Chama cha watengenezaji wa bidhaa za ngozi Tanzania (Tanzania Leather Products Producers Association - TALEPPA) tarehe 2 Septemba, 2025 jijini Dar es Salaam.
Kupitia mradi huo, TALEPPA imedhamiria kuzalisha viatu vya Ngozi vya shule Jozi Milioni 10 kwa mwaka ili kuweza kuhudumia soko la viatu vya shule kwa ufanisi zaidi.
Kwa sasa Tanzania ina takriban wanafunzi milioni 14 ambapo ni soko kubwa la viatu nchini.
Kufanikiwa kwa mradi huu kutaleta mapinduzi makubwa kwenye sekta ya Ngozi nchini na uchumi ujumla ikiwemo kutengeneza ajira za moja kwa moja zaidi ya milioni mbili, kuongeza pato la Taifa kwa wastani wa Shilingi bilioni 300, ongezeko la Kodi kupitia VAT kwa wastani wa Shilingi bilioni 54 kwa mwaka, Kukua kwa sekta ya Ngozi na Mifugo, pamoja na Kujengwa na kuongeza uzalishaji kwa viwanda vikubwa vya ngozi nchini.
TanTrade imeshiriki katika uzinduzi huo ili kuhakikisha uhamishaji wa matumizi ya bidhaa za Tanzania kupitia kampeni ya "Made in Tanzania" na kuhakikisha wazalishaji wa bidhaa za ndani ya nchi ikiwemo bidhaa za ngozi wanajengewa uwezo wa kupata soko la uhakika.
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo alikuwa ni Dkt.Hashil Abdallah, Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara ambaye aliwakilishwa na Bw.Manongi Sempeho, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara, Wizara ya Viwanda na Biashara.