Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

TANTRADE YAKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA WAFANYABIASHARA WA NCHINI QATAR

  • November 28, 2023

27 November, 2023 Doha, Qatar

Katika Mwendelezo wa kutafuta fursa za masoko ya bidhaa za Tanzania kupitia Maonesho ya Dunia ya Matunda na Mboga mboga (Expo 2023 Doha), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imekutana na kufanya mazungumzo ya kibiashara na wawakilishi wa kampuni kubwa mbili za nchini Qatar zilizoonesha nia ya kuwekeza na kununua bidhaa mbalimbali kutoka Tanzania.

Mazungumzo yaliyofanyika kati ya TanTrade na Kampuni ya Al Mona International Trading Co.
Mmiliki wa Kampuni ya Al Mona Int. Co. Bw. Hashim Hassan A. Al Abadi ya nchini Qatar ambayo inajishughulisha na biashara ya uingizaji wa bidhaa za mifugo na vyakula (nyama, kahawa na viungo) kutoka nchi mbalimbali alionesha nia ya kununua bidhaa hizo kutoka Tanzania iwapo atapata ushirikiano wa kutosha kutoka kwenye Mamlaka zinazosimamia uuzaji wa bidhaa nje ya nchi.

Katika mazungumzo yake na Maafisa wa TanTrade, Bw. Hashim alionesha nia ya kuwekeza Tanzania hususan kwenye sekta ya mifugo kwa kuanzisha eneo la kufuga ngombe (Ranch) ili kuwa na uhakika wa malighafi na ubora wa bidhaa za nyama kwa ajili ya masoko ya nje. Pia, mfanyabiashara huyo alionesha nia ya kuwekeza katika kilimo cha chakula cha mifugo ambapo usafirishaji wa bidhaa hizo nje ya nchi itawezesha Tanzania kupata fedha za kigeni.

Mfanyabiashara huyo amekubali mwaliko wa kushiriki katika Siku ya Kitaifa (Tanzania Nationala Day) na Kongamano la Biashara na Uwekezaji (Business and Investment Forum) tarehe 28 na 29 Februari 2024 nchini Qatar. Matukio hayo yanategemewa kuhudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka Serikalini na Sekta Binafsi pamoja na wageni kutoka mataifa mbalimbali yanayoshiriki katika Maonesho haya.

Mazungumzo na Kampuni ya Family Food Center
Kwa upande wa kampuni ya Family Food Center ambayo ni miongoni mwa kampuni zinazomiliki maduka makubwa (Hypermarket) nchini Qatar, mwakilishi wa kampuni hiyo, Bw. Akash Mohan ambaye ni Meneja Uingizaji Bidhaa (Import Manager) alieleza kuwa wapo tayari kununua bidhaa za matunda na mbogamboga kutoka Tanzania pamoja na bidhaa nyingine za matumizi ya nyumbani hasa zile zinazotumika kwa wingi (consumable products) kama vile kahawa, majani ya chai na nyingine.

Kampuni hiyo imehitaji orodha ya bidhaa (product catalogue) zikiwa na maelezo ya aina ya bidhaa ili waweze kuangalia uwezekano wa kuanza kuagiza bidhaa hizo moja kwa moja kutoka Tanzania. Kwa sasa kampuni hiyo hununua nyama ya kondoo kutoka Tanzania. Aidha, Maafisa wa TanTrade waliwahakikishia kuwa itasimamia suala la upatikanaji wa taarifa zote muhimu watakazohitaji ili kuwezesha upatikanaji wa bidhaa hizo.