Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

TANTRADE YAPATIWA UTAALAM WA KUENDELEZA BIASHARA MTANDAO NCHINI CHINA

  • November 3, 2023

Hangzhou, Zhejiang
China
3 Novemba 2023.

Kwa kutambua majukumu ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) ambapo hutekelezwa  sambamba na utekelezaji wa
Ilani ya Chama Tawala, Chama cha Mapinduzi( CCM)  kilitoa fursa kwa TanTrade kupata mafunzo kwa ajili ya kozi ya E-commerce nchini China. Ufadhili huo ulikuwa chini ya Wizara ya Biashara ya China unaotokana na uhusiano mzuri uliopo katika nyanja mbalimbali kati ya nchi hizo mbili.

Katika kozi hii, watendaji wanne, kutoka CCM (2), TanTrade(1) na DART(1) walioteuliwa  kupata mafunzo  mahususi kuhusu
Biashara ya mtandao (E-commerce) kuanzia Oktoba 13 hadi Novemba 3, 2023. Mafunzo haya yaliyofanyika katika mji mkuu wa Teknolojia wa Hangzhou, Jimbo la Zhejiang (wakazi milioni 160) yaliendeshwa na Bodi ya Maendeleo ya Biashara Huria ya Zhejiang(ZFTDB) kwa ufadhili wa Wizara ya Biashara - China.

Washiriki wengine muhimu waliotoka nchi zinazoendelea ni pamoja na Sierra Leone, Oman, Pakistan, Cameroon, Nigeria na Mongolia.

Utaalam huu unatolewa wakati biashara za mtandaoni zinaonekana kushika kasi duniani, hasa baada ya janga la COVID-19 ambapo wafanyabiashara wanatumia mifumo ya kisasa ya mtandao, akili bandia (AI) na mitandao ya kijamii katika kutafuta masoko, bidhaa na wateja na pia kuuza kwa njia za moja kwa moja ni kupitia Utiririshaji wa moja kwa moja wa video.

Wataalam wamepata maarifa mengi juu ya jinsi ya kuunganisha uchumi wa kidijitali, biashara ya mtandaoni na ukuaji wa miji na utalii, mbinu za masoko ya mtandao na bei, uundaji wa vituo vya biashara na miundombinu wezeshi, mauzo na manunuzi kwenye mtandao na kuona kwa wenyewe jinsi masoko ya miji muhimu ya Hangzhouh (teknolojia), Zhuji (vito), Putian (viatu) na Tongxian (mavazi) iliyoko Zhejiang China yanavyofanya kazi kwa ufanisi.
Vile vile, wataalam waliotembelea na kusikiliza mihadhara iliyotolewa na makampuni yanayoongoza katika biashara ya mtandaoni ya mpakani ikijumuisha Alibaba Group, Dahua Technologies, SunHigh na Wensli Silk na Chinagoods.com; ambapo biashara za mtandaoni huchangia zaidi ya asilimia 30 katika mapato ya Jiji la Zhejiang na kuchangia wastani wa yuan bilioni 279 kwa mwaka.

Wataalamu hao wameishukuru Serikali na vyama hivyo kwa kuendelea kukuza Diplomasia ya Uchumi na Biashara na kuahidi kutumia elimu waliyoipata kulitumikia Taifa katika kukuza Biashara na uchumi kwa kuendelea kuwajengea uwezo na ushauri kwa watendaji, Taasisi na wajasiriamali.
------------------------------------
Picha: Tuzo za vyeti kwa maafisa wanne wa Kitanzania na wahitimu wenzao.