Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

TANTRADE YAWAHIMIZA WAFANYABIASHARA WA MCHELE MBARALI KUTUMIA FURSA ZA SOKO HURU LA AFRIKA (AfCFTA)

  • September 7, 2023

MBARALI- MBEYA
05 Septemba, 2023.

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) , imewahimiza wafanyabiashara wa mchele Wilayani mbarali mkoa Mbeya kutumia  fursa za kibiashara kwenye soko huru la Afrika (AfCFTA).
Tantrade imetoa semina hiyo kwa wafanyabiashara wa mchele wilaya ya Mbarali baada ya kufanya semina kama hiyo katika mikoa ya Ruvuma na Njombe.
Lengo la semina hiyo ni kuwajengea uwelewa wafanyabiashara wa mchele juu ya fursa zilizopo katika soko huru la Afrika.
Akifungua Semina hiyo Mkurugenzi  Mtendaji wa Halmashsuri ya Wilaya ya Mbarali Bw. Missana Kwangura, amesema Wilaya ya Mbarali ina kilomita za mraba elfu kumi na sita (16,000) na inazalisha asilimia 30 za mpunga wote unaozalishwa Nchini Tanzania. Uzalishaji huo ufanyika katika skimu za umwagiliaji zilizo  rasmi na zisizo rasmi. Na kwa kutambua hilo
Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya kilimo kwa kuipatia Wilaya ya Mbarali shilingi bilioni 76 kuboresha skimu 6 za umwagiliaji kwa lengo la kuongeza uzalishaji zaidi. Viongozi wa Wilaya ya Mbarali na Wafanyabiashara wa mchele Mbarali wameipongeza Tantrade kwa kuandaa semina hiyo na wameomba kuendelea kupatiwa elimu hususani juu ya namna ya kusafirisha mazao yao nje ya Nchi. Aidha wameliomba shirika la viwango Tanzania (TBS) kuwahi kuwapatia matokeo ya vipimo vya sampuli za bidhaa zao, kwa kuwa matokea ya sampuli hizo huchelewa sana kuwafikia na hivyo kuathiri ufanyaji  biashara nje ya Nchi.
Mpango huu wa mafunzo kwa wafanyabiashar juu ya kutumia fursa za masoko za eneo huru la Afrka ni juhudi za Serikali kuchochea ukuaji wa uchumi na biashara baina ya Nchi wanachama ( intra-Afrika Trade), soko ambalo linatarajiwa kuwa na thamani ya dola za kimarekani trillion 29 ifikapo mwaka 2050.