Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

TANTRADE KUENDELEA KUTOA HUDUMA ZA MAENDELEO YA BIASHARA KWA MAKUNDI MAALUM

  • June 6, 2023

21 Mei, 2023

Na. N. Thomas - TanTrade Dar es Salaam

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imesema kuwa itaendelea kuyaendeleza na kuyapa nguvu makundi maalum katika jamii ili kuhakikisha makundi hayo yanafikia malengo waliyojiwekea. Mojawapo ya makundi hayo ni Jumuhia ya Watu wenye ulemavu inayojulikana kama TUKAWE ( Tuishi Kama Wenzetu) inayosimamiwa kwa ukaribu na TanTrade, inayojishughulisha na utengenezaji wa viatu na uzalishaji wa chaki pamoja na Sabuni.

Hayo yamesemwa na Afisa Biashara mwandamizi kutoka TanTrade Bw. Fredy Liundi kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, wakati akifungua kikao hicho na wanachama walemavu wa kikundi cha TUKAWE amesema kuwa, TanTrade itaendelea kukijengea uwezo kikundi hicho na kuhakikisha kuwa kinaweza kusonga mbele pamoja na kuwa mfano wa kuigwa katika jamii.

“Dhamira yetu njema ni kuendelea kukilea kikundi hiki pamoja na kusapoti shughuli wanazozifanya hususani la kuanzisha kiwanda cha chaki na viatu, hivyo tutawasapoti na kuhakikisha tunawajengea uwezo wa kujiamini ili waweze kujitegemea na kuanzisha kiwanda ambacho kitaweza kuwakomboa wanachama na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na wa nchi kwa ujumla’’ amesema

Hata hivyo, Bw. Liundi amesema katika kikao hicho wamejadili kwa kina changamoto zinazowakabili walemavu hao ambapo ni pamoja na kukosa mitaji ya kujiendeleza na ukosa ujuzi wa kutosha katika kutengeneza bidhaa hizo, ambapo amefafanua kuwa TanTrade itaendelea kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na changamoto hizo.

Naye mwenyekiti wa Tukawe Bw. Mohamed Chilemba amesema kuwa, anaishukuru TanTrade kwa kuendelea kuwasimamia na kuwasaidia katika changamoto zao pamoja na jitihada wanazozionesha za kuwatangaza na kuwashika mkono.

Chilemba ametoa wito kwa taaasisi , kampuni na watu wema waweze kujitokeza na kuwaunga mkono katika shughuli zao za kujikomboa kiuchumi.