Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

TANTRADE YAWAUNGANISHA WAFANYABIASHARA WA MBAO, KARAFUU NA MAZAO YA MIKUNDE NA SOKO LA INDIA.

  • August 25, 2023

...........................

Na. Norah Thomas- TanTrade Dar es salaam.
 18 Agosti 2023.

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeratibu kikao baina ya Bw. Nayan Patel, Mwakiishi wa Heshima wa Tanzania Mumbai- India na Wafanyabiashara wa Mbao, Karafuu na Mazao ya Mikunde nchini kwa lengo la kuwaunganisha wazalishaji nchini na soko la India.

Bw. Patel alieleza kuwa India ina  uhitaji mkubwa wa mbao (teak na pine), karafuu, pilipili manga, mbaazi, dengu na parachichi. Hivyo, ametembelea Tanzania kwa lengo la kuwaaunganisha wauzaji na wasambazaji wa bidhaa hizo na wanunuzi kutoka India.  

‘’Nilianzia biashara nchini Ujerumani ambapo nilitengeneza daraja la kuunganisha  biashara kati ya makampuni makubwa ya India na Ujerumani  na  sasa nipo tayari kuwaunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na India ili kufanya biashara ya mazao haya kwa pamoja na kujipatia masoko na kukuza uchumi wa nchi hizi mbili, pia nipo tayari kuwasaidia wafanyabiashara kutoka Tanzania  wanaoagiza bidhaa India’’ Alisema Bw. Patel Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania Mumbai-India.

Aidha, Afisa Biashara Mkuu kutoka TanTrade Bw. Freddy Liundi  kwa niaba ya  Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade Bi. Latifa M. Khamis alisema Tanzania ina mahusiano mazuri na India na kwa upande wa biashara inauza bidhaa za kilimo, madini na mazao ya misitu. Aidha Tanzania huagiza  madawa, mashine, vipuri, vifaa vya ujenzi kutoka India. Alilisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha mahusiano ya kibiashara na India ili kuongeza zaidi mauzo ya bidhaa zetu katika soko la India.
Kwa upande mwingine Bw. Patel alieleza kuwa India ina fursa kubwa katika viwanda vya ufungashaji na Viwanda vya Madawa ambapo kuna zaidi ya viwanda 500 vinavyotengeneza vifungashio. Hivyo ataendelea kuhamasisha Kampuni za India kuwekeza zaidi Tanzania kutokana  na Tanzania kuwa na mahitaji makubwa ya vifungashio na madawa na kuagiza bidhaa hizo nje ya nchi.

Jumla ya wafanyabiashara ishirini na sita (26) wameshiriki kikao hicho na kuishukuru TanTrade kwa kuwaletea karibu fursa za masoko kutoka  nchi mbalimbali na kuahidi kuchangamkia kutumia fursa hizo kwa manufaa ya biashara zao na Taifa kwa Ujumla.