Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

TANTRADE WAUNGANISHA KAMPUNI ZA TANZANIA NA KAMPUNI YA MAGNIT KUTOKA URUSI

  • September 3, 2023

DAR ES SALAAM
30 AGOSTI, 2023.

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imekutana na kampuni ya Magnit Group kutoka Urusi ambapo muwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu  wa TanTrade, Bw. Emmanuel Miseliya amesema kuwa nchi ya Urusi imekuwa ikishirikiana na Tanzania kwa muda mrefu katika biashara na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali na kubainisha kuwa Tanzania imekuwa ikisafirisha bidhaa Kwenda Urusi  kama vile kahawa, samaki, tumbaku, chai na nyingine nyingi ambapo kwa kipindi cha miaka mitano (2018-2022) Tanzania imekuwa na wastani wastani wa dola za kimarekani milioni 7.86 kwa mauzo  kwenda Urusi  na uagizaji (imports) kutoka  Urusi ni wastani wa dola za kimarekani milioni 112.2 na ambapo bidhaa zilizoagizwa ni zile za uzalishaji na viwanda kama vile vifaa vya umeme, transfoma za umeme na saketi.
Aidha, amewashukuru sana Ubalozi wa Urusi kwa ujio wao kwani wameweza kujadiliana na makampuni  ya Tanzania kuhusu Biashara ya bidhaa za Kilimo kwa mazao kama vile  korosho, alizeti, viazi mviringo, na kwa upande wa matunda ni pamoja na vile ndizi, nanasi, embe, papai n.k

Kwa upande mwingine, Mwambata-Biashara na Uchumi  wa Ubalozi wa Urusi Bw. Nikita  amesema kuwa Ubalozi wa Urusi unataka kuendeleza sera yake ya kufanya Biashara  na Kuwekeza katika Bara la Afrika, pia ameona washiriki wengi katika nchi ya Tanzania kwa pamoja wataweza kuimarisha vitega uchumi katika nchi zote mbili, na amesisitiza suala la kujenga msimamo ambapo italeta faida kubwa katika nchi ya Tanzania na Urusi.

Pia ameshukuru kwa kuwepo kwa mkutano huo kwani wataweza kuunganisha kampuni mbalimbali za kutoka Urusi na Tanzania na kupanga jinsi ya kuimarisha mawasiliano kwaajili ya kubadilishana taarifa mbalimbali kuhusu biashara na kujenga mikakati ya kupandisha uchumi.

Pia Bw. Michael kutoka Urusi ambae amekuwa na uzoefu wa kufanya biashara nchini Tanzania kwa mazao ya matunda kama vile ndizi na pia korosho amesema kuwa anatamani kushirikiana na kampuni za Tanzania katika usafirishaji wa aina nyingine za matunda kama vile papai, nanasi, maembe, parachichi na pasheni kwa lengo la kujenga biashara kubwa ndani na nje ya nchi ya Urusi pamoja na Tanzania. Amemaliza kwa kusisitiza kuwa bidhaa zinaposafirishwa zitiliwe umakini kwa kutoifadhiwa kwa mda mrefu, mazao kama vile ndizi huwa zinaharibika kwa haraka hivyo anatazamia kuwauzia wateja wake bidhaa iliyo safi na salama. Hivyo, kuhitaji kampuni ya uhakika ya lojistiki kutoka Tanzania