Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

TANTRADE NA SHIRIKA LA MAHUSIANO YA KIMATAIFA LA UJERUMANI (G.I.Z) WAJIPANGA KUWEZESHA WAFANYABIASHARA MIPAKANI.

  • July 21, 2023


________________________
Na Norah Thomas- TanTrade Dar es salaam.

8 Mei, 2023 

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) na Shirika la GIZ zimekubaliana kushirikiana katika uwezeshaji wa Sekta ya biashara hususan kwenye eneo la Wafanyabishara wanawake na vijana wanaovuka mipaka. Aidha, eneo lingine taasisi hizo mbili zimeonesha nia ya kushirikiana ni eneo muhimu la taarifa za biashara na kurahisisha wafanyabiashara kuzipata kwa njia rahisi.

Hayo yalisemwa tarehe 8 Mei 2023 na Bw. Fortunatus Mhambe, Kaimu Mkurugenzi wa Ukuzaji Biashara wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) alipokuwa akizungumza katika Mkutano uliofanyika kwenye ofisi za TanTrade zilizopo Uwanja wa Maonesho wa Mwl. J. K Nyerere, Barabara ya Kilwa Dar es Salaam, ambapo amesema kuwa Uwezeshaji huo unalenga zaidi Miradi ya Maendeleo kwa Wafanyabiashara Wajasiriamali wadogo waliopo maeneo ya mipakani ili kuwarahisishia kufanya biashara kwa ufanisi na kukuza biashara zao na uchumi kwa ujumla pamoja na kuwezesha kwenye ukusanyaji wa hatua za uingizaji na uuzaji wa mazao na bidhaa mbalimbali nje ya nchi kwenye Mfumo wa Trade Information Portal.

Naye Meneja wa Mradi kutoka GIZ Bi. Claudia Hofmann amesisitiza kuwa, nchi ya Ujerumani ipo tayari kuimarisha uhusiano wa kibiashara na Tanzania kwa kuwawezesha wafanyabiashara wadogo waliopo mpakani hususan Wanawake na Vijana, hivyo imekuja na mpango mkakati wa kuwasaidia Wafanyabiashara hao kwa kuwajengea uwezo wa kufanya biashara zao kwa uhuru na ufanisi zaidi.

Bi Claudia alimalizia kwa kusema haya “programu hii inalenga kukuza biashara ndani na nje ya Tanzania hivyo tumejipanga kutoa mafunzo na kuwapa wadau wetu nafasi za kuonesha bidhaa zao, kuwajengea uwezo wa kufanya biashara kwa uhuru na ufanisi zaidi na pia tunatoa nafasi kwa wadau kupata masoko mbalimbali ya ndani na nje ya nchi”.