TANTRADE NA KOTRA WAKUBALIANA KUSHIRIKIANA KATIKA BIASHARA NA UWEKEZAJI.
- August 25, 2023

Mapema leo Tarehe 25 Agosti 2023 TanTrade imefanya kikao kazi na Ujumbe kutoka Taasisi ya biashara Korea Kusini, KOTRA DSM (Korea Trade-Investment Promotion Agency) chenye lengo la kutaka ushirikiano wa kibiashara na Uwekezaji na kubaini fursa zinazopatikana katika nchi ya Tanzania na Korea ili kuzitumia ipasavyo kwa lengo la kukuza na kuendeleza uchumi wa nchi hizo mbili.
Kikao hicho kimefanyika katika ofisi ya TanTrade barabara ya Kilwa Dar es salaam, pia kimehudhuliwa na Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade Bi. Latifa Khamis, pamoja na Mkurugenzi Mkuu Kamishna wa Biashara kutoka KOTRA Bw. Wohn Jun Young Kwa kushirikiana na ujumbe kutoka TanTrade na KOTRA.
Katika Kikao hicho Bi. Latifa amesema kwamba, Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia TanTrade ipo tayari kutoa ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji na Taasisi hiyo ili kupanua wigo wa biashara na kuwasaidia Wafanyabiashara kutoka nchi hizo mbili kuweza kutegemeana kibiashara na kukuza uchumi.
Naye Bw. Whon Jun Young amesema kuwa KOTRA imejitolea katika ukuaji thabiti wa biashara na upanuzi wa soko huku kukiwa na mabadiliko ya dhana katika uchumi wa dunia na mfumo wa kutambua fursa katika soko la kimataifa hivyo KOTRA Inapenda kujenga ushirikiano na Tanzania ili kukuza biashara pamoja na kuchochea mabadiliko aswa kwenye sekta ya viwanda.