Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

TANTRADE NA CTI KUANDAA MAONESHO YA KIMATAIFA YA BIDHAA ZA VIWANDA VYA TANZANIA.

  • June 13, 2023

Na. Norah Thomas-- TanTrade, Dar es salaam.

------------------

12 JUNI,2023.

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) na  Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (C.T.I), wametia  saini Mkataba wa  Makubaliano ya kufanya kazi kwa pamoja ili kuwezesha Maonesho ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania kuendelea kuwa yenye tija na kuongeza mapato kwa mfanyabiashara mmoja mmoja pamoja na Taifa kwa ujumla.

Mkutano huo umefanyika  leo tarehe 12 Juni, 2023  katika ofisi za C.T.I zilizopo jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na  Mkurugenzi  Mkuu wa TanTrade Bi. Latifa  M. Khamis  na Mkurugenzi Mtendaji wa C.T.I,  Bw. Leodgar Tenga walioambatana na Wataalamu kutoka pande zote mbili. 

Akizungumza katika Mkutano huo, Bi. Latifa amesema lengo kubwa la makubaliano hayo ni kuongeza nguvu katika kufanikisha Maonesho ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania ili zilete masoko ya kitaifa na Kimataifa.

‘’Kuna tukio kubwa tunatarajia kulifanya mwaka huu, tumeamua kufanya Maonesho  makubwa ya Bidhaa za viwanda yatakayojulikana kama  ‘Tanzania Manufacturer Expo’ ambayo yatajumuisha viwanda vya ndani na nje ya Tanzania. Tofauti na kipindi cha nyuma, mwaka huu  tutafanya ‘International Expo’ kwa kushirikiana na C.T.I, pia tutakuwa na mikutano ya kuunganisha wafanyabiashara mbalimbali, tutahakikisha uwekezaji wa sekta ya viwanda unakuwa na unafanikiwa kwa viwango vya juu’’. Alisema.

Aidha, aliendelea kufafanua  kuwa,
‘Mkataba huu unaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha uchumi wa nchi unakuwa kwa kasi zaidi, kwa kutangaza bidhaa za Tanzania pamoja na viwanda vya ndani ya nchi ili kuchochea uzalishaji na kupata masoko ya ndani na nje ya nchi.’’

Naye Mkurugenzi wa C.T.I Bw. Leodgar Tenga amesema kuwa, tukio hilo ni la muhimu sana kwa wenye viwanda, hivyo wanaishukuru  TanTrade kwa kukubali kuungana na kufanya kazi kwa pamoja kwani ni matumaini yao kuwa  Mkataba huo utasaidia sana kuunga  mkono jitihada za  Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kufungua masoko na nchi  hususani  kwenye suala la Uwekezaji wa viwanda.

‘’Tunatoa wito kwa wadau wetu kutuunga mkono kwenye jambo hili la kitaifa kwani Maonesho ya mwaka huu yatakuwa na mabadiliko ya hali ya juu kwa kuwa tunategemea Kufanya  Maonesho makubwa  zaidi na ya kuvutia uwekezaji kwani  tumejipanga kuhusisha zaidi ya makampuni 500 ya wenye Viwanda  kutoka ndani na nje ya nchi kuja kufanya, hivyo tunaomba wananchi na wadau wetu watuunge mkono kwenye jambo hili la Kitaifa’’ alisema.
Kwa mwaka huu Maonesho ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania (Tanzania Manufacturer Expo) yanatarijiwa kufanyika tarehe 4 -6 Octoba, 2023.