RAIS DKT. MWINYI AFUNGA MAONESHO YA 47 YA SABASABA (47 DITF 2023)
- July 26, 2023

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk
Hussein Mwinyi amesema Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam
(DITF) yameonekana kuwa ya kuvutia na ya
kipekee, kutokana na maandalizi ya hali ya juu pamoja na wingi wa ubora wa
bidhaa na huduma zinazoonyeshwa.
Kwa maboresho zaidi,
aliagiza mamlaka zinazohusika kufuta minyororo ya ukiritimba isiyo ya lazima
kwa biashara na uwekezaji ili kustawi na kuvutia washiriki zaidi, pia amezitaka
Taasisi zinazosimamia biashara kuhakikisha zinaondoka urasimu na kuwawezesha
Wafanyabiashara nchini kwa kuwawekea Mazingira rafiki ya Biashara zao.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo tarehe 13 Julai 2023, katika
Uwanja wa Mwl. JK Nyerere Dar es salaam alipokuwa akifunga Maonesho ya 47 ya
Biashara ya Kimataifa mahalufu kama SabaSaba ambapo alisema ili kupunguza gharama za kufanya
biashara, kero za tozo zinapaswa kufutwa pia Serikali ya Tanzania Bara na
Visiwani zitashirikiana katika
kuhamasisha ukuaji wa Biashara na Uwekezaji kwa kufanyia kazi maoni ya
Wafanyabiashara nchini.
Vile vile, alishauri wazalishaji wa ndani ambao wamepokea
maagizo kutoka kwa makampuni ya kigeni kuzingatia viwango vinavyohitajika.
Pia Dkt Mwinyi aliongeza kuwa
Mwaka huu, jumla ya makampuni 3,500 yakiwemo 267 kutoka nje ya nchi
yalishiriki katika maonyesho hayo, hatua aliyoitaja kuwa ni mafanikio kutokana
na mipango inayoendelea kutekelezwa ili kuboresha mazingira ya biashara.
Maonesho yameongozwa na Kauli Mbiu ya ‘’Tanzania ni Mahala
sahihi pa Biashara na Uwekezaji’’ ikiwa inaenda sambamba na utekelezaji wa
Majukumu ya TanTrade.
Akizungumza katika hafla ya ufungaji wa Maonesho hayo
Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade Bi. Latifa M. Khamis amesema kuwa idadi ya washiriki imeongezeka kutoka
washiriki 3,200 mwaka 2022 hadi kufikia washiriki 3,500 mwaka 2023, sawa na
ongezeko la asilimia 9%. Kati ya hao, Washiriki wa ndani ni 3,243 ukilinganisha
na 2,880 mwaka 2022 sawa na ongezeko la
asilimia 18%. Kadhalika Washiriki wa nje walikuwa 267 kutoka nchi 17
zinazojumuisha, China, Ghana, India, Indonesia, Japan, Kenya, Singapore, Syria,
UAE, Uturuki, Iran, Rwanda, Burundi, Uganda, Algeria, Misri, Korea, Malaysia na
Pakistan.
Vilevile alisema zaidi
ya Watembeleaji 259,966 walifanikiwa kuingia katika Uwanja wa Maonesho wa Mwl.
J. K. Nyerere kwa ajili ya mahitaji mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi
ukilinganisha na Watembeleaji 265,957 mwaka 2022.
‘’Maonesho ya 47
yamefanikisha kuingia kwa jumla ya makubaliano tisa (9) ya ushirikiano (MOU)
katika sekta na maeneo mbalimbali yakiwemo maeneo ya Ununuzi wa Pamba ya
Tanzania tani 30,000 kwa mwaka baina Bodi ya Pamba na makampuni kutoka nchi ya
Algeria, Ununuzi wa Katani ya Tanzania kati Bodi ya Katani na Makampuni kutoka
nchi ya India na Ushirikiano wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Morogoro
(SUA) na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Chaudhary Charan Singh, Haryana-India kwenye
maeneo mahususi ya kubadilishana wanafunzi (Exchange Programmes), mafunzo kwa
njia ya mtandao (Online Programmes) na mafunzo ya kawaida (Offline Programmes)
ambapo masomo yaliyopewa kipaumbele ni Kilimo (Agriculture), Biashara ya Kilimo
(Agribusiness), Teknolojia kwa viumbe hai (Biotechnology), Sayansi ya Chakula
(Food Science) n.k.’’ Alisema.
Aidha Bi. Latifa aliongeza kuwa, Kupitia jukwaa hili la
Maonesho, Washiriki wameweza kufanya mauzo ya bidhaa na huduma yenye thamani ya
shilingi milioni 3,820.70 ukilinganisha na shilingi milioni 3,592.50 Mwaka
2022. Vilevile, kupitia Mikutano ya kibiashara (B2B) iliyokutanisha Wadau
kutoka sekta mbalimbali ndani na nje ya nchi, imewezesha kufanyika kwa
mazungumzo na makubaliano ya kibiashara ambapo oda za bidhaa zenye thamani ya
shilingi bilioni 16.98 zimepatikana. Nikuhakikishie, TanTrade itaendelea
kushirikiana na wadau hawa ili kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa
makubaliano hayo na kuwezesha mauzo ya bidhaa hizo.
Pia alifafanua kuwa Maonesho
hayo yalifanikiwa kutoa jumla ya kazi za muda 11,687.
“Tuliweza kutoa ajira za muda katika shughuli zilizokuwa
zikiendelea hapa viwanjani, ikiwa ni pamoja na kufanya usafi, usafiri, mapambo,
vyakula, migahawa,” alisema Bi Latifa.