Made in Tanzania fahari ya Tanzania
- November 20, 2024
20 Novemba, 2024
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) Bi Latifa M. Khamis amezindua rasmi shindano la rajamu(chapa) ya Made in Tanzania kwa kutoa wito kwa wabunifu wa picha na wasanii wa Tanzania kutumia fursa hii ya kuunda utambulisho wa Taifa letu na kuonyesha ubunifu, fahari na uwezo ulio ndani ya bidhaa na huduma zetu za ndani , katika Mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo tarehe 20 Novemba, 2024 katika ofisi za TANTRADE zilizopo katika Kiwanja cha JK Nyerere, barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam.
Aidha Bi Latifa ameeleza kuwa shindano hili ni kuunda rajamu (chapa) itakayotambulika na ya kipekee ambayo itakuwa rajamu ya Taifa letu ambapo itawakilisha kwa ufahari bidhaa na huduma za Tanzania hapa nchini na Kimataifa, na kuwa alama ya ubora, imani na fahari kwa nchi yetu.
Vilevile ametabainisha kuwa lengo kuu ni kuhakikisha kuwa bidhaa za Tanzania zinafahamika zaidi katika masoko ya Kimataifa kwa utambulisho wenye nguvu wa chapa na kuimarisha ushindani wetu, kuongeza mahitaji ya bidhaa na huduma za Tanzania ikiwa ni pamoja na kuvutia uwekezaji katika uchumi wetu.