MADE IN TANZANIA NI CHANZO CHA UKUAJI WA BIASHARA NCHINI PROFESA MBAMBA.
- January 8, 2026
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Profesa Ulingeta O. L. Mbamba, leo ametembelea banda la Made in Tanzania katika Maonesho ya 12 ya Kimataifa ya Biashara ya Zanzibar yanayoendelea katika Uwanja wa Dimani, Fumba.
Katika ziara hiyo, Prof. Mbamba ameipongeza TanTrade kwa juhudi zake madhubuti katika kukuza bidhaa za ndani kupitia nembo ya Made in Tanzania. Amesema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa taifa wa kuimarisha ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Aidha, ametoa wito kwa wazalishaji na wafanyabiashara kote nchini kuchangamkia fursa ya kutumia nembo ya Made in Tanzania, akieleza kuwa ni nyenzo muhimu ya kuaminika inayotambulika kimataifa na inayosaidia kuongeza thamani ya bidhaa, upatikanaji wa masoko mapya, na kuimarisha utambulisho wa bidhaa za Tanzania duniani.