Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

WADAUWA MAONESHO WAAMASISHA WAFANYABIASHARA NA WATEMBELEAJI KUJIANDAA NA MAONESHO YA 47 YA SABASABA(DITF 2023)

  • July 21, 2023









..................................

Na. Norah Thomas- TanTrade Dar es salaam.
 2 Juni, 2023.


Wadau wa Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa (DITF) maarufu kama Sabasaba wamesema Maonesho ya mwaka huu ni ya kipekee kwa kuwa yanatoa fursa kwa Taasisi, kampuni wajasiriamali na watu mbalimbali kushiriki katika Maonesho hayo.

Wamesema hayo tarehe 2  Juni,  2023 katika Uwanja wa Maonesho ya Mwl. JK Nyerere Dar es salaam wakati wakizungumza na   Waandishi wa habari, ambapo Mkurugenzi wa Kampuni Tanzakwanza  bw. Francis Daudi amesema wana mabanda maalum Expo Village lengo likiwa ni kuonesha huduma zinazopatikana katika Sekta mbalimbali Nchini.


“Kampuni yetu kwa kushirikiana na TanTrade tumeandaa Banda maalum la Expo Village kwa lengo la kukutanisha Sekta nane ambazo ni Madini, Kilimo, Mazingira, Uwekezaji Michezo na zingine kwa ajili ya  kujadili changamoto na fursa zilizopo, pia   SabaSaba Expo Village imelenga kuwavutia Wawekezaji wa ndani na nje na kuonesha rasilimali watu iliyopo nchini'' amesema.

Kwa upande wake Msanii wa Filamu Nchini Bw.Salim Ahmed (Gabo) amesema  atakuwepo katika Banda la SabaSaba Expo
Village ambapo ataonesha filamu yake mpya aliyoitengeneza baada ya kuwezeshwa mkopo na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, aidha Bw.Gabo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuthamini na kuwawezesha Wasanii.

Naye Mtafiti na Mgunduzi wa vyakula vya asili kutoka kampuni ya Dorikin, Profesa Dorcas Kibona amesema kampuni yake intakuwepo na kuonesha bidhaa zinazotokana na kilimo hai na kuwashirikisha vijana katika fursa mbalimbali zinazotona na kilimo Hai.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Machinga Mkoa wa Dar es Salaam, Namoto Yusuph amesema wanataka kuwa na kituo maalum cha pamoja cha kuzalisha bidhaa.

“Kuna machinga wengi ni wazalishaji wa bidhaa kama batiki, sandozi na bidhaa mbalimbali tunahitaji kuwa na kituo maalum ili iwe rahisi kuwaunganisha na wataalamu namna ya kutengeneza bidhaa zenye viwango na Mamlaka ya Viwango Tanzania(TBS) ikague bidhaa hizo,”amesema Yusuph huku akiwaomba machinga kujitokeza kwa wingi kwenye maonyesho ya sabasaba'' alisema.