Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

KONGAMANO LA AFRO WORLD AGRI FOOD 2023 LAFUNGULIWA RASMI

  • August 11, 2023



Mkurugenzi Mkuu Wa TanTrade Bi. Latifa  M. Khamis akimwakilisha Mhe.Dkt Ashatu K. Kijaji, Waziri wa, Viwanda na Biashara amefungua  Kongamano la Kilimo na Chakula la Afrika (Afro World Agri Food Conference, Exhibition and Awards) linalofanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 10 – 12 Agosti, 2023 Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Kongamano hilo linaenda sambamba na maonesho na mikutano ya ana kwa ana ya wafanyabiashara (B2B) wa bidhaa na mazao mbalimbali zikiwemo mazao ya jamii ya kunde kama maharage, njegere na  mbaazi, ufuta,  soya, alizeti, nafaka zikiwemo ngano na mchele , kahawa, kokoa na chai.

Katika hotuba yake, Bi. Latifa amewapongeza waandaaji wa kongamano kwa kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa Kongamano hilo na kuwaomba kuwa kwenye kongamano la mwaka ujao waichague tena Tanzania kuwa mwenyeji wa kongamano hilo. 

Aidha aliwakaribisha wafanyabiashara waliotoka nje ya Tanzania kufanya biashara na kuwekeza kwenye sekta ya kilimo nchini kwa kuwa kuna mazingira rafiki ya ufanyaji biashara na  Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kutengeneza na kuboresha mazingira ya biashara pamoja na miundombinu ili kurahisisha ufanyaji wa biashara.
Kadhalika, Bi. Latifa aliongeza kuwa Tanzania ni nchi ya kimkakati kwa uwekezaji na biashara kutokana na kuwa na bandari ambayo inahudumia nchi zaidi ya 7. 

Aidha Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC)  yenye idadi ya watu takribani milioni 470. Tanzania pia ni miongoni mwa nchi za Afrika ambazo zimeridhia mkataba wa AfCFTA unaomaanisha kuwa mfanyabiashara sasa anaweza kupata soko la zaidi ya watu bilioni 1.3 katika bara la Afrika.

Kongamano hilo la Afro World Agri Food Conference, Exhibition and Awards linawaunganisha wafanyabiashara na wakulima wa Tanzania na nje ya Tanzania kubadilishana fursa mbalimbali zikiwemo fursa za soko, teknolojia na ujuzi.

Mkurugenzi Mkuu pia aliwaasa wafanyabiashara na wadau mbalimbali kuwasiliana na TanTade kwaajili ya kuunganishwa na fursa za biashara na pia aliwakaribisha wageni waliotoka nje ya nchi kutembelea maeneo mbalimbali ya utalii nchini kama Ngorongoro, Serengeti, Kilimanjaro na Zanzibar.