Habari

Imewekwa: 06/04/2019

NAFAKA YA TANZANIA KUPENYA UKANDA WA MASHARIKI NA KATI YA NCHI

NAFAKA YA TANZANIA KUPENYA UKANDA WA MASHARIKI NA KATI YA NCHI

Wafanyabiashara wa nafaka nchini wametakiwa kujipanga kuuza nafaka ikiwemo zao la mahindi katika nchi za Rwanda,Burundi,Comoro,Kongo na Zambia.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Bw Edwin Rutageruka alipokuwa akifungua Kikao cha Wadau wa Nafaka kilichofanyika tarehe 5 Aprili,2018 katika ofisi za TanTrade, Dar es Salaam.

Bw Rutageruka amesema, kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki TanTrade imepokea maombi ya sekta binafsi kutoka nchi ya Rwanda ya kununua kiasi cha tani 102,000 za Mahindi kwa kipindi cha mwaka 2019,ambapo ujumbe wa sekta binafsikutoka nchini humo upo tayari kufanya ziara nchini ili kukutana na wafanyabiashara mbalimbali wa nafaka ikiwemo mahindi.

“kwa sisi Serikali tunawategemea Bodi ya Mazao Mchanganyiko aweze kufanya biashara lakini zaidi zaidi sekta binafsi,kwahiyo ni vizuri kila mtu aseme uwezo wake ili tuwaruhusu wafanyabiashara kutoka Rwanda waje,na wenzetu wa Burundi wapo tayari kuja” alisema Rutageruka

Aliongeza kuwa kuna uhitaji wa kiasi cha tani 100,000 za Mahindi kutoka nchi ya Burundi, tani 3,000 za Mahindi kutoka nchi ya Zambia na tani 3,000 za Mahindi kutoka Visiwa vya Comoro.

Bw.Rutageruka ametoa wito kwa wafanyabiashara wa nafaka wa sekta binafsi kukusanya mahindi katika maghala maalum ili iwe rahisi kuwafikia mara tu yanapohitajika.

“Sekta Binafsi wanamahindi lakini changamoto kubwa yamesambaa katika maeneo mbalimbali kwa viwango vidogo vidogo”

Kwa upande wake Afisa Programu,Baraza la nafaka la Afrika Mashariki(EAGC) Bw.Junior Ndesanjo ameishukuru Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania(TanTrade) kwa kutoa taarifa hizo muhimu za biashara na ameiomba serikali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi kukusanya taarifa sahihi za ubora,bei,upatikanaji na mahali soko linapopatikana.

Bw.James Mbasira ni mfanyabiashara wa nafaka ameshauri serikali kuanzisha magala ya nafaka ambayo yatakuwa yanaongozwa na Vyama Vya Ushirika ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa za uwepo wa nafaka.