Habari

Imewekwa: 08/11/2019

RAIS WA CHINA MHE XI JINPING AVUTIWA NA KOROSHO NA TANZANITE

RAIS WA CHINA MHE XI JINPING AVUTIWA NA KOROSHO NA TANZANITE

Rais wa China Mhe Xi Jinping afungua rasmi maonesho ya Pili ya Kimataifa ya Bidhaa za nje na kuahidi kwamba Nchi yake itafungua milango zaidi kwa bidhaa za nje kuingia katika soko la China. Katika hafla hiyo viongozi wa Mataifa 64 walihudhuria akiwemo Rais wa Ufaransa Mhe Emmanuel Macron, Mawaziri Wakuu wa Jamaica; Serbia na Greece. Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Innocent Bashungwa.

Aidha baada ya kufungua maonesho hayo Rais wa China ametembelea Mabanda ya nchi (5) yakiwemo mabanda ya Ufaransa; Ugiriki; Serbia; Jamaica na Tanzania.

Katika ziara ya kutembelea Banda la Tanzania Rais Xi Jinping alifuatana na Waziri Mkuu wa Jamaica; Greece na Serbia na kupokelewa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Innocent Bashungwa.

Balozi wa Tanzania Ndugu Mbelwa Kairuki alitoa maelezo juu ya bidhaa mbalimbali za kilimo na madini zinazopatikana nchini Tanzania na vivutio vya utalii. Aidha, Balozi Kairuki aliwasilisha salaam za Rais wa Tanzania Mhe Dk John Pombe Magufuli kwa Rais wa China.

Kwa upande wake Rais wa China ameipongeza Tanzania kwa kushiriki katika maonesho ya Pili ya Kimataifa ya Bidhaa za Nje na ametuma salaam za pongezi kwa Mhe Rais Magufuli kwa kuimarisha mahusiano ya kiuchumi kati ya Tanzania na China. Aidha, Rais Xi alivutiwa zaidi na bidhaa ya korosho za Tanzania na madini ya Tanzanite ambapo alitaka kufahamu zaidi juu ya upatikanaji wa bidhaa hizo katika soko la China.Maonesho ya Kimataifa yataendelea hadi tarehe 10 Novemba 2019.