TANTRADE YATOA MAFUNZO MAALUM YA BIASHARA NA MASOKO KWA CHAMA CHA WAOKAJI TANZANIA (TBA)
- May 14, 2026
Dar es Salaam, 13 Mei 2026
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeendesha mafunzo maalum kwa Chama cha Waokaji Tanzania (TBA) ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uwezo wa wafanyabiashara wa sekta ya uokaji kutumia fursa za masoko ya kikanda na kimataifa. Hatua hii inalenga kuongeza ujuzi na kuimarisha ushindani wa washiriki katika kukuza biashara zao ndani na nje ya nchi.
Mafunzo hayo ya siku mbili yamejikita katika kuwajengea uwezo washiriki kuhusu mbinu za kisasa za biashara, matumizi sahihi ya Rajamu ya Taifa (Made in Tanzania), na namna ya kuongeza thamani ya bidhaa ili ziweze kushindana katika masoko ya kimataifa. Washiriki pia wamepata elimu juu ya mikakati ya uuzaji, usimamizi wa ubora, na uendelevu wa biashara, sambamba na fursa za ushirikiano wa kikanda kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Kwa upande wa TanTrade, mafunzo haya yameonesha dhamira ya taasisi hiyo katika kuimarisha sekta ya biashara kwa kuunganisha wadau wa ndani na masoko ya kimataifa. Aidha, yamekuwa jukwaa la kujadili changamoto zinazokabili sekta ya uokaji na kutoa suluhisho za kitaalamu ili kuongeza tija na ajira. Hatua hii inatarajiwa kuchochea ukuaji wa sekta ya viwanda vidogo na vya kati, na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika ushindani wa kibiashara kimataifa.