TANTRADE YAHAMASISHA USHIRIKI WA MAONESHO YA MIAKA 50 KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA WAFANYAKAZI
- May 4, 2026
TANTRADE
YAHAMASISHA USHIRIKI WA MAONESHO YA MIAKA 50 KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA
WAFANYAKAZI
Dar es Salaam, 1
Mei 2026
Mamlaka ya Maendeleo
ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeungana na wafanyakazi duniani kuadhimisha Siku
ya Wafanyakazi Duniani, tukio linalotambua mchango mkubwa wa wafanyakazi
katika kukuza uchumi wa taifa na ustawi wa jamii. Maadhimisho hayo yamefanyika
katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, yakihudhuriwa na viongozi
wa serikali, wadau wa sekta binafsi, pamoja na wananchi kutoka makundi
mbalimbali.
Katika maadhimisho
hayo, TanTrade imetumia jukwaa hilo kuhamasisha wadau wa biashara kushiriki na
kudhamini Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam 2026 (DITF 50
Jubilee), yanayoadhimisha Miaka 50 ya mafanikio na historia ya maonesho
hayo. Maonesho haya yameendelea kuwa chachu ya maendeleo ya sekta ya
biashara kwa kutoa nafasi ya kuonesha bidhaa na huduma, kukuza ubunifu,
kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa, pamoja na kufungua milango ya
fursa za masoko ya ndani na nje ya nchi.
Aidha, TanTrade
imesisitiza kuwa wafanyakazi ni nguzo ya msingi katika kufanikisha
majukumu ya taasisi hiyo, hususan katika kuratibu maonesho ya biashara,
kuunganisha wafanyabiashara na fursa mbalimbali za uwekezaji, na kuendeleza
ubunifu wa kitaifa. Kupitia juhudi, maarifa na ubunifu wa wafanyakazi, taasisi
imeendelea kuchochea ukuaji wa sekta ya biashara, kuongeza ushindani wa bidhaa
za Tanzania kimataifa, na kuimarisha taswira ya taifa katika majukwaa ya
biashara ya dunia.
TanTrade imewahimiza
wadau wote serikali, sekta binafsi, na wananchi kuunga mkono maonesho haya ya
kihistoria, ambayo si tu yanadhihirisha mchango wa wafanyakazi, bali pia
yanajenga msingi wa uchumi imara na endelevu kwa vizazi vijavyo.