TANTRADE YAHAMASISHA BIDHAA ZA MADE IN TANZANIA KUFIKIA MASOKO YA KIMATAIFA KUPITIA CONSUMER CHOICE AWARDS
- September 29, 2026
29 Septemba 2026, Dar es Salaam
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imewahamasisha wazalishaji, wajasiriamali na wafanyabiashara kutumia jukwaa la Consumer Choice Awards 2026 kutangaza bidhaa za Tanzania, kujenga uhusiano wa kibiashara na kutafuta masoko mapya nje ya nchi.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Hoteli ya King Jada, Dar es Salaam, Meneja wa Ukuzaji wa Biashara wa TanTrade, Bw. Deo Shayo, amesema jukwaa hilo litajumuisha mikutano ya biashara kwa biashara (B2B) itakayowaunganisha washiriki wa Tanzania na wadau wa masoko ya kimataifa. Amehimiza wazalishaji kutumia alama rasmi ya Made in Tanzania ili kuongeza utambulisho wa bidhaa zao.
Bw. Shayo amesema bidhaa zinazofanya vizuri katika soko la ndani zinahitaji pia kutangazwa na kuunganishwa na washirika wa biashara ili kupata nafasi katika masoko ya nje. TanTrade itaendelea kutoa elimu na ushauri kwa wafanyabiashara kuhusu ukuzaji wa biashara na kuongeza ushindani wa bidhaa zao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Consumer Choice Awards Africa, Dkt. Diana Laizer, amesema maandalizi yanaendelea vizuri na amewataka wajasiriamali, wazalishaji na wafanyabiashara kujisajili. Amesema jukwaa la biashara litafanyika tarehe 27 Novemba 2026, likifuatiwa na hafla ya utoaji wa tuzo tarehe 28 Novemba 2026, jijini Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu.
Zaidi ya wafanyabiashara 150 kutoka Tanzania wanatarajiwa kushiriki. Kupitia ushirikiano wake na Consumer Choice Awards Africa, TanTrade inalenga kuwasaidia washiriki hao kutangaza bidhaa zao chini ya alama ya Made in Tanzania, kufanya miadi ya kibiashara na kufungua fursa katika masoko ya kimataifa.