Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

TANTRADE NA BARAZA LA MCHELE (RCT) WATOA SEMINA YA MAUZO NJE KWA WAFANYABIASHA MBARALI

  • July 21, 2023

_________________
Mei 16, 2023
Mbarali- Mbeya

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa kushirikiana na Baraza la Mchele Tanzania (RCT) wametoa semina  kwa Wafanyabiashara kuhusu upatikanaji wa soko na taratibu za usafirishaji wa zao la Mchele  katika eneo la Halmashauri ya Mbarali.
Washiriki wa semina hii ni pamoja na viongozi waliowakilisha wafanyabiashara wa mchele kutoka Tandale (mwenyekiti akiwakilisha wafanyabiashara 1,055), Tandika, Temeke, na mbagala inayohudumia masoko ya Mkuranga, Rufiji na Kilwa. Wadau wengine waliohudhuria ni Mbeya Rice, KTC Kilombero Rice, MTC Morogoro wakiwakilisha vikundi vya wasindikaji wa mchele na wadau wa Igawa na Ubaruku.

Lengo la Semina hiyo lilikuwa ni kutoa uelewa kuhusu Biashara za Mchele  katika Soko la Ndani na kuwaunganisha Wasindikaji na wadau wa Masoko na walaji wengi (pamoja na DSM) ili waweze kuwa na mahusiano ya kibiashara na kutengeneza Biashara endelevu.

Akifungua Semina hiyo Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Mhe. Kanali Dennis Mwila amewasisitiza wasindikaji na wafanyabiashara wa zao hilo kujipanga kimkakati na kuhudumia fursa za masoko ndani na nje badala ya kutulia na kulalamikia ukosefu wa soko.

Naye, mtaalamu kutoka TanTrade Bw.Deo Shayo alibainisha kuwa maeneo ambayo mchele na nafaka nchini Tanzania kwa ujumla wake unaendelea vizuri ni katika masoko ya miji ya kibiashara ikiwemo Dsm na Arusha na kwa upande wa masoko ya nje yanayoonekana zaidi ni Kenya, Burundi, Uganda, Congo DRC, Zambia na Rwanda. Kufafanua taratibu na hati muhimu kwa biashara za nje (mauzo ya nje)
Bw.Shayo ametoa ushauri kwa wafanyabiashara kuchangamkia fursa mpya za biashara zinazojitokeza katika Soko Huria la Afrika (AfCFTA) ambapo wigo wa kutoa huduma ni mkubwa huku kukiwa na nchi zaidi ya 50 kwa unafuu wa ushuru wa forodha na pia watumiaji wengi zaidi. Pia, wafanyabiashara wametakiwa kushiriki katika matukio ya Maendeleo ya Biashara ya TanTrade yakiwemo Maonesho ya Sabasaba kuanzia tarehe 28 Juni hadi 13 Julai 2023 ili kujitangaza.
Kwa upande wa Baraza la Mpunga wameahidi kuendelea kuwasaidia wazalishaji wa zao la mpunga katika masuala ya kushauri sera rafiki kwa kushirikiana na serikali ili kuimarisha uzalishaji na biashara ya zao la mpunga nchini.

Aidha wafanyabiashara wameishukuru RCT kupitia wawakilishi wake Bw.Geofrey Rwiza na Leoncia Salakana pamoja na Serikali kwa ujumla kwa kuona umuhimu wa kuinua Biashara nyingi za Mpunga kwani wameajiri watu wengi na pia kuongoza katika mauzo ya nje hivi karibuni. Kwa hiyo kuomba matatizo yao ya mara kwa mara ikiwa ni pamoja na malipo wanapovuka kutoka Halmashauri moja kwenda nyingine yapunguzwe au kuondolewa kabisa.

Mpango huu wa mafunzo na kuwakutanisha wadau ni sehemu ya jitihada zinazofanywa na Baraza la Mpunga Tanzania kwa kushirikiana na wafadhili na Mamlaka za Serikali katika kuboresha mnyororo wa thamani wa mchele na bidhaa husika.