Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

TANTRADE NA BALOZI MTEULE KOREA YA KUSINI KUIMARISHA USHIRIKIANO WA BIASHARA KATI YA KOREA KUSINI NA TANZANIA

  • April 23, 2026

TANTRADE NA BALOZI MTEULE KOREA YA KUSINI KUIMARISHA USHIRIKIANO WA BIASHARA KATI YA KOREA NA TANZANIA

23 Aprili 2026, Dar es Salaam
_____________________________________

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeendelea kutekeleza jukumu lake la kuunganisha Tanzania na masoko ya kimataifa. Leo, Balozi Mteule wa Tanzania nchini Korea ya Kusini, Mhe. Noel E. Kaganda, amefanya ziara katika ofisi za TanTrade kwa mazungumzo ya kimkakati yanayolenga kupanua wigo wa biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Korea ya Kusini.

Katika mazungumzo hayo, TanTrade imeeleza kuwa bidhaa za Tanzania zimekuwa zikivuma katika soko la Korea ya Kusini, hususan madini, tumbaku, ufuta, mwani, korosho na mazao ya jamii ya kunde. Kwa upande mwingine, Korea ya Kusini imeendelea kusambaza bidhaa za viwanda na teknolojia nchini Tanzania, jambo linaloonyesha ushirikiano wa kibiashara na kuleta manufaa kwa pande zote mbili.

Aidha, TanTrade imechukua nafasi hiyo kumkaribisha Mhe. Balozi pamoja na wadau wa biashara kutoka Korea kushiriki katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026), tukio kubwa la kitaifa linalotarajiwa kuvutia washiriki kutoka zaidi ya nchi 30. Ushiriki wa wadau wa Korea utakuwa chachu ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kuongeza uwekezaji wa moja kwa moja, na kuendeleza teknolojia na ubunifu katika sekta mbalimbali za uzalishaji.

TanTrade imesisitiza kuwa ushirikiano huu ni fursa ya kipekee kwa wafanyabiashara wa Tanzania kujipenyeza zaidi katika soko la Asia Mashariki, huku ikiwahimiza wadau wa ndani kuongeza uzalishaji na ubora wa bidhaa ili kukidhi mahitaji ya kimataifa.