TAARIFA KWA UMMA TANZANIA NA RWANDA KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA SEKTA ZA BIASHARA, UCHUKUZI NA NISHATI
- May 4, 2026
TAARIFA KWA UMMA
TANZANIA NA RWANDA KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA SEKTA ZA BIASHARA, UCHUKUZI NA
NISHATI
Dar es Salaam 03
Mei, 2026;
Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo amempokea
Ikulu jijini Dar es Salaam Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame,
aliyewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku moja.
Rais Dkt. Samia na
mwenzake, Rais Kagame wamefanya mazungumzo ya ana kwa ana, na baadaye kuongoza
mazungumzo rasmi ya uwili yaliyohusisha ujumbe wa nchi zote mbili, na kufuatiwa
na mazungumzo na waandishi wa habari. Viongozi hao wamejadili hatua za
kuimarisha ushirikiano katika biashara na uwekezaji, uchukuzi na miundombinu,
nishati, ulinzi na usalama, uhamiaji, pamoja na uratibu wa misimamo ya nchi
hizo mbili katika masuala ya kikanda na kimataifa.
Akizungumza baada ya
mazungumzo hayo, Rais Dkt. Samia amesema Tanzania na Rwanda zimeendelea kujenga
uhusiano wa undugu, ujirani mwema na urafiki wa kihistoria, unaoakisi
mshikamano wa muda mrefu kati ya wananchi wa pande zote mbili. Rais Dkt. Samia
amesema biashara kati ya Tanzania na Rwanda imeendelea kukua na kufikia thamani
ya shilingi bilioni 644 mwaka 2025. Amesema kuanzia mwaka 1990 hadi mwezi
Machi, 2026, Mamlaka ya Uwekezaji Tanzania imesajili miradi 42 ya uwekezaji
kutoka Rwanda yenye thamani ya dola za Marekani milioni 325.5, iliyozalisha
ajira 2,225 kwa Watanzania. Pamoja na hatua hiyo, Rais Dkt. Samia amesema nchi
zote mbili zimekubaliana kuongeza kasi ya kuondoa changamoto za kibiashara,
ikiwemo vikwazo visivyo vya kikodi, ili kupanua biashara na uwekezaji, na
kutumia kikamilifu fursa za soko la pamoja la Afrika Mashariki na Soko Huru la
Biashara la Afrika.
Katika uchukuzi na miundombinu, Rais Dkt. Samia amesema
takribani asilimia 70 ya shehena za Rwanda hupitia bandari za Tanzania, na
kwamba Tanzania itaendelea kuweka mazingira bora ya kuhudumia shehena hizo,
ikiwemo huduma maalum katika bandari, matumizi ya Bandari ya Dar es Salaam na
Bandari ya Tanga, pamoja na maeneo ya kuhifadhi mizigo.
Marais hao pia
wamejadili uendelezaji wa miundombinu ya reli na barabara, ikiwemo mradi wa
reli ya Isaka hadi Kigali, unaolenga kuharakisha usafirishaji wa bidhaa na
kuongeza ufanisi wa biashara kati ya nchi hizo mbili. Katika nishati, viongozi
hao wamejadili Mradi wa Umeme wa Maporomoko ya Rusumo, unaozihusisha Tanzania,
Rwanda na Burundi, wenye uwezo wa kuzalisha megawati 80, pamoja na makubaliano
ya kuuziana umeme kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Shirika la
Umeme la Rwanda (REG), kwa ajili ya kuchochea shughuli za kiuchumi kwa manufaa
ya nchi zote mbili.
Kwa upande wake, Rais Paul Kagame amemshukuru Rais Dkt.
Samia na Watanzania kwa mapokezi mazuri, akisema Tanzania ni mshirika muhimu wa
Rwanda, hususan katika biashara na usafirishaji kupitia bandari zake
zinazoiunganisha Rwanda na masoko ya kimataifa. Rais Kagame amesema Tanzania na
Rwanda zinapaswa kuimarisha msingi imara wa uhusiano uliopo kwa kuendeleza
ushirikiano katika maeneo ya kimkakati ili kukuza biashara, kuendeleza miradi
ya pamoja na kusukuma mbele ajenda ya maendeleo ya nchi hizo mbili. Aidha,
amesema Rwanda itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Tanzania katika kuimarisha
ushirikiano ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Umoja wa Afrika na majukwaa
mengine ya kimataifa, kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote mbili.
Ziara ya Rais
Kagame nchini inadhihirisha nafasi muhimu ya Tanzania katika biashara na
ushirikiano wa kikanda, kama mshirika wa karibu na lango la biashara kwa nchi
jirani, huku makubaliano yaliyofikiwa yakitarajiwa kuongeza biashara,
kurahisisha usafirishaji na kufungua fursa zaidi kwa wananchi wa nchi zote
mbili.
Bakari S. Machumu
Mkurugenzi wa Mawasiliano
ya Rais, Ikulu