KATIBU MKUU WA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA ATEMBELEA MABANDA YA MAONESHO, APONGEZA UBUNIFU NA UKUAJI WA WAJASIRIAMALI
- November 3, 2026
02 Novemba 2026 | Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Balozi Waziri Rajab Salum, ametembelea mabanda mbalimbali ya wajasiriamali, wazalishaji na washiriki wa maonesho yanayofanyika kuelekea uzinduzi wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda na Sera ya Maendeleo ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (SMEs), akijionea bidhaa, huduma na ubunifu unaochangia maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Katika ziara hiyo, Mhe. Balozi Salum alipata fursa ya kutembelea mabanda ya taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, sekta binafsi, pamoja na wajasiriamali kutoka maeneo mbalimbali nchini, ambapo alijionea bidhaa zinazozalishwa nchini na kupokea maelezo kuhusu shughuli zinazotekelezwa katika kukuza viwanda, biashara na ujasiriamali.
Akizungumza na washiriki wa maonesho hayo, Mhe. Balozi Salum alieleza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayochochea ukuaji wa viwanda na biashara kwa lengo la kuongeza ajira, kuimarisha ushindani wa bidhaa za Tanzania na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya uchumi wa Taifa. Alisisitiza kuwa wajasiriamali wadogo na wa kati ni nguzo muhimu katika mnyororo wa thamani wa uzalishaji na biashara, hivyo wanastahili kupewa nafasi na uwezeshaji unaohitajika ili kukuza shughuli zao.
Aidha, alizipongeza taasisi na wadau wanaoshiriki maonesho hayo kwa kuendelea kuonesha bidhaa na huduma bunifu zinazodhihirisha uwezo wa Watanzania katika uzalishaji, uchakataji na utoaji wa huduma zenye viwango vinavyokubalika katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Maonesho hayo yanatoa fursa kwa wananchi, wafanyabiashara, wawekezaji na wadau wa maendeleo kujifunza kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya viwanda na biashara, pamoja na kupata taarifa kuhusu sera, mipango na programu mbalimbali zinazolenga kuimarisha ushindani na ukuaji wa sekta hizo.
Maonesho yalianza rasmi leo tarehe 02 Novemba 2026 na yataendelea hadi tarehe 04 Novemba 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete (JKCC), jijini Dodoma. Kilele cha maonesho hayo kitakuwa uzinduzi wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda na Sera ya Maendeleo ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (SMEs), unaotarajiwa kuongozwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Salvio Kapinga (Mb).
Uzinduzi wa sera hizo unatarajiwa kuweka msingi imara wa kukuza uzalishaji wenye ushindani, kuongeza thamani ya bidhaa za ndani, kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji, pamoja na kuwajengea uwezo wajasiriamali ili waweze kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania.