Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

BALOZI WA PALESTINA AFANYA MAZUNGUMZO NA MAMLAKA YA MAENDELEO YA BIASHARA TANZANIA (TANTRADE) KUHUSU USHIRIKI WA SABASABA 2026

  • April 14, 2026

BALOZI WA PALESTINA AFANYA MAZUNGUMZO NA MAMLAKA YA MAENDELEO YA BIASHARA TANZANIA (TANTRADE) KUHUSU USHIRIKI WA SABASABA 2026
———————————
14 Aprili 2026, Dar es Salaam

Balozi wa Palestina nchini Tanzania, Mheshimiwa Salam Abu Sharar, amefanya ziara katika ofisi za Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa mazungumzo ya maandalizi ya ushiriki wa taifa lake katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF – Sabasaba 2026).

Katika mazungumzo hayo, Balozi alieleza kuwa Palestina iko tayari kushiriki kikamilifu katika maonesho hayo makubwa ya kibiashara, akibainisha kuwa ushiriki huo utakuwa chachu ya kuitangaza nchi yake kimataifa, kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na kidiplomasia, pamoja na kuongeza uelewa wa umma kuhusu utamaduni, biashara na fursa zilizopo nchini Palestina. Aidha, alisisitiza kuwa ushiriki wa Palestina katika DITF 2026 ni sehemu ya mkakati wa taifa lake wa kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na nchi za Afrika Mashariki, hususan Tanzania.

Kwa upande wake, uongozi wa TanTrade ulimkaribisha rasmi Balozi na kumpatia mwongozo wa taratibu za kupata nafasi ya maonesho, sambamba na ushauri wa namna bora ya kuandaa na kushiriki kwa ufanisi katika tukio hilo. Uongozi pia ulisisitiza dhamira ya TanTrade ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kupitia maonesho ya Sabasaba, ambayo yamekuwa jukwaa muhimu la kukuza biashara, uwekezaji na diplomasia ya kiuchumi.