MAONESHO YA BIASHARA YA KIMATAIFA YA NAIROBI YAFUNGULIWA RASMI; BANDA LA TANZANIA LANG'ARA
- September 30, 2026
30 Septemba, 2026, Nairobi, Kenya
Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Nairobi (Nairobi International Trade Fair) yaliyoanza tarehe 28 Septemba, 2026 katika Viwanja vya Maonesho vya Jamhuri Jijini Nairobi, yamefunguliwa rasmi leo tarehe 30 Septemba, 2026 na Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo wa Serikali ya Jamhuri ya Kesnya Mhe. Mutahi Kagwe.
Akiwa katika banda la Tanzania, Mhe. Kagwe, amevutiwa na ubora wa bidhaa mbalimbali pamoja na huduma zinazotolewa katika banda hilo, zikiwemo bidhaa za ngozi, asali na nafaka.
Kagwe amesema Tanzania ina fursa kubwa ya kupata masoko ya bidhaa za nafaka na nyinginezo zenye ubora zinazozalishwa nchini Tanzania.
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeratibu ushiriki wa kampuni tatu za Tanzania zinazozalisha bidhaa chakula, ngozi na asali, ambazo ni KOM Food Products, Woiso Original Products na Asilia African Honey.
Ushiriki wa TanTrade katika maonesho haya unalenga kutangaza bidhaa zinazozalishwa nchini kupitia rajamu ya Made in Tanzania, kutafuta masoko na kuunganisha wazalishaji na fursa za biashara katika soko la ukanda wa Afrika Mashariki na Kimataifa.
Aidha, miongoni mwa taasisi nyingine zinazoshiriki masonesho hayo ni pamoja na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ambayo inatangaza miradi yake mbalimbali ya kimkakati ikiwemo jengo la ghorofa 22 lililopo Nairobi, nchini humo.
Maonesho haya yanatarajiwa kufungwa rasmi tarehe 4 Oktoba 2026.