Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

BWAWA LA UMEME LA MWL. NYERERE (JNHPP) LAFUNGUA UKURASA MPYA WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI

  • August 23, 2026


Rufiji | 22 Agosti, 2026

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua rasmi Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115, hatua inayoweka msingi muhimu wa kuimarisha upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa shughuli za uzalishaji, viwanda, biashara na uwekezaji nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Rais amesisitiza dhamira ya Serikali kuendelea kuimarisha Gridi ya Taifa na miundombinu ya kusafirisha umeme ili nishati inayozalishwa kupitia mradi huo iwafikie wananchi na maeneo ya uzalishaji na kuchochea zaidi shughuli za kiuchumi nchini.

Kukamilika kwa JNHPP kumeongeza uwezo wa Tanzania wa kuzalisha umeme hadi kufikia Megawati 4,646, wakati mahitaji ya juu ya Gridi ya Taifa yakiwa Megawati 2,271, hivyo Taifa kuwa na ziada ya Megawati 2,375. Ziada hiyo inatoa nafasi kubwa zaidi ya kukidhi mahitaji ya viwanda na uwekezaji mpya, sambamba na kufungua fursa ya biashara ya umeme na nchi jirani.

Kwa sekta ya viwanda na biashara, upatikanaji wa umeme mwingi na wa uhakika ni kichocheo muhimu cha kuongeza uzalishaji viwandani, kupunguza changamoto za uzalishaji zinazotokana na upungufu wa nishati, kuimarisha uchakataji na uongezaji thamani, kuvutia uwekezaji na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani, kikanda na kimataifa.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Salvio Kapinga (Mb.), ambaye alishiriki katika hafla hiyo, amekuwa akisisitiza umuhimu wa upatikanaji wa umeme mwingi na wa uhakika katika kuvutia uwekezaji. Hivyo kukamilika kwa JNHPP kunatoa fursa kubwa kwa sekta ya viwanda na biashara kutumia nishati hiyo kuongeza uzalishaji, kuendeleza viwanda vipya na kupanua shughuli za biashara na uwekezaji.

Aidha, Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya kusafirisha umeme, ikiwemo njia ya Kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma yenye urefu wa kilomita 345, pamoja na miundombinu ya vituo vya Chalinze na Zuzu, hatua inayolenga kuwezesha umeme wa JNHPP kuwafikia watumiaji katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo katika kongani za viwanda zinazojengwa katika kila wilaya nchini.

Kukamilika kwa mradi huu wa kimkakati kunaiweka Tanzania katika nafasi nzuri zaidi ya kutumia nishati kama kichocheo cha uchumi wa viwanda, biashara, uwekezaji na kuongeza thamani ya rasilimali zinazozalishwa nchini, sambamba na kuimarisha ushindani wa Taifa katika kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.