WAZIRI KAPINGA AHIMIZA UWEZESHAJI WA WAJASIRIAMALI KWA AJILI YA KUKUZA VIWANDA NA BIASHARA
- November 3, 2026
02 Novemba 2026 | Dodoma
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Salvio Kapinga (Mb), amewataka wadau mbalimbali nchini kuendelea kuwaunga mkono na kuwajengea uwezo wajasiriamali, akisisitiza kuwa mchango wao ni muhimu katika kukuza sekta ya viwanda na biashara ambayo kwa sasa inachangia takribani asilimia 15 ya Pato la Taifa.
Mhe. Kapinga ametoa wito huo wakati akifungua maonesho yanayoshirikisha Wizara ya Viwanda na Biashara, taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo pamoja na wadau wa sekta binafsi. Maonesho hayo ni sehemu ya maandalizi ya uzinduzi wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda na Sera ya Maendeleo ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (SMEs), unaotarajiwa kufanyika tarehe 04 Novemba 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete (JKCC), jijini Dodoma.
Akizungumza katika maonesho hayo, Waziri Kapinga amesema kuwa uwezeshaji wa wajasiriamali ni mkakati muhimu katika kuimarisha uzalishaji wa bidhaa, kuongeza thamani ya bidhaa za ndani na kupanua fursa za masoko. Amesema hatua hizo zinachangia ukuaji wa biashara na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Katika ziara yake kwenye banda la Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Mhe. Kapinga alipokea maelezo kutoka kwa Afisa Biashara Mwandamizi, Bw. Tito Nombo, kuhusu juhudi zinazofanywa na Mamlaka hiyo katika kuwajengea uwezo wafanyabiashara na wajasiriamali, kuwapatia taarifa za masoko pamoja na kuwaunganisha na wanunuzi wa ndani na nje ya nchi.
Aidha, Waziri Kapinga alielezwa kuhusu elimu inayotolewa na TanTrade juu ya taratibu za usajili na manufaa ya matumizi ya nembo ya “Made in Tanzania”. Elimu hiyo inalenga kuimarisha utambulisho wa bidhaa na huduma za Tanzania, kuongeza imani ya walaji na kukuza ushindani wa bidhaa hizo katika masoko ya ndani na kimataifa.