KONGAMANO LA ZIWA TANGANYIKA LAZAA MATUNDA, GAVANA (DRC) ATETA NA TANTRADE KUHUSU BIASHARA NA TANZANIA
- April 22, 2026
KONGAMANO LA ZIWA
TANGANYIKA LAZAA MATUNDA, GAVANA (DRC) ATETA NA TANTRADE KUHUSU BIASHARA NA
TANZANIA
21 Aprili 2026, TanTrade HQ, Dar es Salaam
Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zimefungua ukurasa mpya wa kuimarisha ushirikiano wa kibiashara unaolenga kuimarisha biashara ya kikanda na kuongeza uwekezaji baina ya mataifa haya mawili. Hatua hii imejidhihirisha baada ya maafisa kutoka DRC kutembelea ofisi za TanTrade kwa mazungumzo zaidi, kufuatia kumalizika kwa Kongamano la Ziwa Tanganyika lililofunguliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mwigulu Nchemba, na ambalo lilishirikisha Wakongo wengi waliovutiwa na maonyesho hayo. Kongamano hilo limekuwa jukwaa la majadiliano ya kimkakati na kubadilishana mawazo ya kibiashara kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.
Mkurugenzi Mkuu wa
TanTrade, Dkt. Latifa Khamis, alisisitiza kuwa TanTrade ni daraja la
biashara kati ya Tanzania na mataifa ya nje, akiwakaribisha wafanyabiashara
kutoka DRC kutumia fursa zilizopo nchini. Alieleza kuwa Tanzania imejipanga
kutumia lango la magharibi kupitia Kigoma katika kuimarisha biashara
kwenye nchi za Ushoroba wa Kati kwa kurahisisha huduma za usafirishaji na
upatikanaji wa bidhaa za viwandani na vyakula, ili kuongeza mchango wa sekta
binafsi katika uchumi wa kikanda. Aidha, alibainisha kuwa TanTrade itaendelea
kushirikiana na taasisi za kikanda na kimataifa ili kuhakikisha kuwa Tanzania
inabaki kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki
na Kati.
Kwa upande wake, Gavana
wa Jimbo la Kivu Kusini (Bukavu), Profesa Jean-Jacques Purusi Sadiki,
amewahimiza wafanyabiashara wa Tanzania kuwekeza nchini DRC, akibainisha kuwa
kuna nafasi nyingi za kibiashara na uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo
kilimo, viwanda, nishati, madini, na huduma za kijamii. Aliongeza kuwa serikali
ya DRC itaendelea kuhakikisha mazingira salama na rafiki kwa wawekezaji, ili
kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kukuza biashara ya kikanda. Gavana pia
alisisitiza umuhimu wa kuendeleza miradi ya pamoja ya miundombinu, hususan
barabara na bandari, ili kurahisisha mtiririko wa bidhaa na huduma kati ya
mataifa haya mawili.
Aidha, Gavana
ameishukuru TanTrade kwa mwaliko wa kuja kushiriki Maonesho ya 50 ya
Biashara ya Kimataifa SabaSaba, na amesema ataambatana na wafanyabiashara
wakubwa ili kupata fursa zaidi za biashara katika maonesho hayo yatakayoanza
tarehe 28 Juni 2026. Ameeleza kuwa ushiriki wa DRC katika maonesho haya
utakuwa ishara ya mshikamano wa kikanda na utatoa nafasi ya kuendeleza
majadiliano ya kimkakati kuhusu biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi.
Ziara hii imeweka
msingi wa ushirikiano wa muda mrefu, ambapo Tanzania na DRC zinatarajiwa
kuimarisha mtandao wa biashara kupitia mipango ya pamoja, kubadilishana uzoefu
wa kiuchumi, na kuendeleza miradi ya kipaumbele inayolenga ustawi wa wananchi
wa pande zote mbili. Hatua hii pia inatarajiwa kuongeza mchango wa sekta
binafsi katika ajira, mapato ya serikali, na ukuaji wa uchumi wa kikanda.
Kwa ujumla, Kongamano
la Ziwa Tanganyika limekuwa chachu ya kuimarisha diplomasia ya kiuchumi,
likitoa dira mpya ya ushirikiano wa kikanda na kuonyesha dhamira ya Tanzania na
DRC katika kujenga uchumi imara, shirikishi na endelevu.