Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

SABASABA YACHANGIA FURSA ZA BIASHARA NA UWEKEZAJI ZAIDI YA SH TRILIONI 129 KWA MIAKA 50

  • July 7, 2026

Dar es Salaam, 6 Julai 2-26

 Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imetangaza kuwa Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF – Sabasaba) yamekuwa chachu kubwa ya maendeleo ya kiuchumi, yakizalisha fursa za biashara na uwekezaji zenye thamani ya takribani shilingi trilioni 129.31 katika kipindi cha nusu karne. Mafanikio haya yamechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha nafasi ya Tanzania katika biashara za kikanda na kimataifa, huku yakionyesha mchango wa maonesho hayo kama jukwaa la kipekee la kuunganisha wadau wa maendeleo.

Akizungumza katika hafla ya maadhimisho ya miaka 50 Maonyesho ya Kimataifa ya Sabasaba, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Dkt. Latifa Khamis, alieleza kuwa maonesho hayo yamekuwa daraja muhimu la kuwaleta pamoja wafanyabiashara, wawekezaji na wadau wa sekta mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi. Alisisitiza kuwa mchango wa DITF katika kukuza uchumi wa taifa ni dhahiri, kwani yamekuwa yakitoa fursa za ajira, kuongeza uzalishaji, na kuimarisha taswira ya Tanzania kama kitovu cha biashara na uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Dkt. Khamis alifafanua kuwa safari ya maonesho haya ilianza kupitia Board of Internal Trade na Board of External Trade, kabla ya kuunganishwa na kuunda TanTrade ya sasa, ambayo ipo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara. Tangu kuanzishwa kwake, TanTrade imeendelea kuratibu juhudi za kukuza biashara na masoko ya bidhaa za Tanzania, ikilenga kuimarisha ushindani wa bidhaa za ndani katika masoko ya kimataifa.

Aidha, alibainisha kuwa maadhimisho ya Jubilei ya Dhahabu yanalenga kutambua na kuthamini mchango wa washiriki, wadhamini, washirika wa maendeleo na wadau mbalimbali waliotoa msaada mkubwa katika kufanikisha maonesho haya kwa kipindi cha miaka 50. Alisema kuwa mchango wa wadau hao umekuwa msingi wa mafanikio ya Sabasaba, na umechangia kuifanya Tanzania kuwa na maonesho yenye hadhi ya kimataifa yanayovutia nchi zaidi ya 20 kila mwaka.

Kwa mujibu wa Dkt. Khamis, maonesho ya Sabasaba yamekuwa si tu jukwaa la biashara, bali pia chombo cha diplomasia ya kiuchumi, yakisaidia kuimarisha uhusiano wa kikanda na kimataifa kupitia ushiriki wa mataifa mbalimbali. Aliongeza kuwa maadhimisho haya ni fursa ya kutathmini tulipotoka, tulipo na tunapoelekea, ili kubaini changamoto na fursa mpya za maendeleo.

Kwa jumla, mchango wa Sabasaba katika kipindi cha miaka 50 unadhihirisha nafasi yake ya kipekee katika historia ya biashara ya Tanzania. Kupitia maonesho haya, taifa limeweza kujenga msingi imara wa uchumi wa viwanda, kuimarisha sekta binafsi, na kuendeleza taswira ya Tanzania kama kitovu cha biashara na uwekezaji barani Afrika.