SABASABA YA MIAKA 50: JUKWAA LA BIASHARA, UBUNIFU NA UWEKEZAJI NUSU KARNE
- June 12, 2026
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mh. Sixtus Mapunda, amefanya ziara katika viwanja vya Maonesho ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (Sabasaba) kujionea maandalizi ya Maonesho ya 50 yanayoandaliwa na TanTrade.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ziara hiyo, Mh. Mapunda amesema ameridhishwa na hatua kubwa zilizofikiwa katika maandalizi hayo, akibainisha kuwa maonesho ya mwaka huu yatakuwa ya kipekee kutokana na kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.
Ameeleza kuwa Maonesho ya Sabasaba yameendelea kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa biashara, uwekezaji na ubunifu nchini, huku yakitoa fursa kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kuonesha bidhaa na huduma zao. Aidha, amepongeza TanTrade kwa juhudi za kuboresha miundombinu, usalama na huduma mbalimbali ili kuwahudumia washiriki na wageni kwa ufanisi.
Mh. Mapunda ametoa wito kwa wananchi, taasisi na sekta binafsi kutumia fursa ya Maonesho ya 50 ya Sabasaba kujifunza, kufanya biashara na kujenga mitandao ya kibiashara itakayochochea maendeleo ya uchumi. Vilevile, amesisitiza washiriki kukamilisha upambaji wa mabanda yao na wananchi kutembelea kwa wingi.
Aidha Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Dk. Latifa Khamis, akitoa maelezo kuhusu mipango ya taasisi amesema maandalizi ya Maonesho ya 50 yanaendelea vizuri, huku nchi 23 zikithibitisha ushiriki wao. Aidha, zaidi ya makampuni 258 ya kimataifa na makampuni 776 ya ndani tayari yamejiandikisha kushiriki, jambo linalodhihirisha kuongezeka kwa imani ya wadau wa biashara na uwekezaji katika maonesho haya makubwa ya kihistoria.
Dk. Latifa amebainisha kuwa Sabasaba ya mwaka huu itakuwa jukwaa muhimu la kutangaza bidhaa na huduma za Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa, kuvutia masoko mapya na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya wafanyabiashara, wawekezaji na taasisi mbalimbali. Ongezeko la washiriki ni ishara ya kukua kwa mazingira ya biashara na uwekezaji nchini pamoja na nafasi ya Tanzania katika uchumi wa dunia.
Aidha, maonesho haya yataambatana na kampeni maalum ya kuhamasisha matumizi ya bidhaa zenye nembo ya “Made in Tanzania”, pamoja na programu za biashara, ubunifu na uwekezaji zitakazoongeza thamani ya maonesho. Dk. Latifa amesisitiza kuwa mafanikio ya bidhaa za Tanzania kupenya katika masoko ya kimataifa yanatoa fursa kwa wazalishaji kuongeza uzalishaji, ubora na ushindani wa bidhaa zao.
Amehitimisha kwa kuwataka wadau ambao bado hawajakamilisha maandalizi yao kufanya hivyo mapema ili kunufaika kikamilifu na fursa zitakazotolewa na Maonesho ya 50 ya Sabasaba