Habari

Imewekwa: 05/06/2018

WAZALISHAJI WA BIDHAA ZA NGOZI WAJENGEWA UWEZO.

WAZALISHAJI WA BIDHAA ZA NGOZI WAJENGEWA UWEZO.

Wazalishaji thelathini (30) wa bidhaa za ngozi kutoka Chama cha Wazalishaji wa Bidhaa za Ngozi Tanzania (TALEPPA) wamejengewa uwezo kwa kupewa mafunzo ya siku tatu yaliyoratibiwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade).

Mafunzo hayo yaliyoongozwa na Bw Emmanuel Miselya, Kaimu Mkurugenzi wa Uendelezaji Biashara kutoka TanTrade amesema kuwa lengo la kuwajengea uwezo wazalishaji wa bidhaa za ngozi ni kuwasaidia kuwa na ushindani katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

‘’Sekta hii ina rasilimali nyingi na ikitumiwa vizuri kwa kushirikiana na wazalishaji wenyewe Tanzania itakuwa na viwanda vingi vya ngozi na bidhaa zake na wananchi watapata ajira itakayowaongezea kipato kikubwa kwa sababu kuna fursa kubwa ya masoko ndani na nje ya nchi hivyo kuongeza wigo wa kodi”, alisema Bw Miselya.

Aidha aliongeza kwa kueleza kuwa TanTrade itahakikisha inatoa mafunzo kwa wazalishaji wa bidhaa zenye muelekeo wa viwanda ili rasilimali za nchi zitumike vizuri na kuweza kuvutia ongezeko la uwekezaji nchini.

Nae, Bw Johnson Kiwia, Afisa Viwango kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), amewashauri wazalishaji wa bidhaa za ngozi kuzingatia kutumia malighafi iliyothibitishwa na taasisi hiyo ilikuwapa ujasiri wa kufanya biashara ndani na nje ya nchi na kuweza kumudu ushindani wa soko.

Kwa niaba ya wanufaika wa mafunzo hayo, Bw.Timoth Funto, Katibu wa Chama cha Wazalishaji wa Bidhaa za Ngozi Tanzania (TALEPPA) ameeleza kuwa kupitia mafunzo hayo wamepata ujuzi wa masoko yatakayowawezesha kutatua changamoto ya namna ya kusimamia biashara zao ili kukidhi hitaji la msingi lililokuwa linawatatiza katika uzalishaji.

Mafunzo ya awamu ya tatu yamejikita kwenye uzalishaji bora wa bidhaa zenye viwango, kuzingatia usalama mahala pa kazi na namna ya kubuni bidhaa zenye mvuto na kuendana na mitindo ya kisasa yenye kupendwa na watumiaji wengi.

Taasisi zilizoshiriki kuwajengea uwezo wazalishaji hao ni Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia kitengo cha KAIZEN, TBS, VETA, OSHA na DIT kampasi ya Mwanza.